Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Jenista Mhagama ambaye ni mgombea ubunge kwa tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM)Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma amesema Serikali kupitia Wizara ya kilimo itaanza kutoa mikopo ya kilimo kwa vijana, wenye lengo la kuwainua kiuchumi na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za kilimo cha kisasa chenye tija.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Lilahi jana iliyopo jimbo la Peramiho halmashauri ya Wilaya ya Songea vijijini,kwenye mkutano wa kampeni wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu na kuwaomba wananchi waweze kumchagua mgombea wa kiti cha Urais kupitia CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge pamoja na Diwani wa kata hiyo Simon Kapinga.

Alisema kuwa mwaka huu kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi wamejipanga kutoa mikopo kwa vikundi ambavyo vinataka kuzalisha kwa wingi mazao ya biashara na chakula hivyo amewataka vijana wa kitongoji cha Kitinginyi kujipanga ili mikopo hiyo wasiikose.
“Mkawe watu wa mwanzo wa kupata mikopo ya kilimo, lakini habari nyingine njema kwa wale wanaotaka kuanza kusindika mahindi,kutokuuza mahindi kama mahindi,kuanza kuuza unga wa sembe na leo tunapoenda kujenga barabara yetu ya kwenda Mkenda kwa rami.
” Tunataka kufungua soko la kimkakati mpakani mwa Tanzania na Msumbiji itakuwa ni fursa kwa wanakitinginyi kwenda kuuza kule unga unaotokana na zao la mahindi”alisema Mhagama.

Alisema fursa nyingine serikali tayari imeweka utaratibu wa kukopesha vijana wanaotaka kuanzisha vituo ama mashine za kusaga mahindi na kutengeneza unga na kwenda kuuza mpakani mwa Tanzania na Msumbiji hivyo amewataka wajipange kwani anawafahamu kuwa ni wachapakazi na wana uwezo wa kuyafanya hayo.
“Tunatamani kuhakikisha Jimbo letu la Peramiho, halmashauri yetu ya Wilaya inakwenda kibiashara zaidi,inafanya mambo ambayo itasaidia uchumi wa mwananchi mmoja mmoja lakini uchumi wa Kata,uchumi wa Wilaya na uchumi wa Mkoa wa Ruvuma nao unapiga hatua na unasonga mbele,ndugu zangu wana Kitinginyi,ndugu zangu wana Makwaya nawaomba mtupatie kura za kishindo wagombea wa CCM kwa nafasi ya Urais,Ubunge na udiwani” alisema Mhagama.
Awali akiomba kura mgombea udiwani wa kata hiyo ya Lilahi Simon Kapinga amemshukuru Dkt. Samia Suluu Hassan pamoja na mgombea ubunge Jenista Mhagama kwani wamefanyia mambo makubwa sana kwenye kata hiyo ikiwemo miradi ya maji,umeme,Afya lakini ameomba fedha halmashauri ya Wilaya ya Songea kwaajiri ya ukarabati wa majengo ya shule za msingi Makwaya,Lilahi pamoja na Aboudjumbe ambazo zimejengwa mwaka 1968 na majengo yake yamechakaa sana.

Naye mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea vijijini Thomas Masolwa amewaomba wananchi wa kata hiyo kutofanya makosa ya kupigia vyama vingine kura badala yake wawapigie kura wagombea wa CCM kwa maendeleo zaidi ambapo amesema kuwa Ilani ya CCM 2025/2030 imeandika miradi yote ikiwemo usambazaji wa umeme kwenye baadhi ya vitongoji ambavyo havijafikiwa sambamba na usambazaji wa maji kwenye vitongoji na miundombinu ya barabara.


