Mgombea Ubunge wa Viti Maalum kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Jesca Magufuli, amesema kuwa kila Mtanzania anashuhudia mafanikio makubwa yaliyotekelezwa na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameyasema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais kupitia CCM uliofanyika Oktoba 12, 2025, wilayani Bukombe, mkoani Geita.
Amesema kuwa Dkt. Samia ni kiongozi mchapakazi na jasiri, akibainisha kuwa uthubutu wake ulidhihirika mara baada ya kuchukua kiti cha urais katika kipindi kigumu baada ya kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Ameeleza kuwa licha ya changamoto za kipindi hicho, kwa kipindi cha miaka minne Dkt. Samia ameweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati iliyoanzishwa na mtangulizi wake, huku akiibua na kuanzisha miradi mipya ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Aidha, amebainisha kuwa miradi mingi iliyotekelezwa na Dkt. Samia inajieleza yenyewe, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambapo sasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ni safari ya saa tatu pekee, sambamba na kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la JPM (Busisi–Mwanza) ambalo limeongeza ufanisi wa usafiri na biashara Kanda ya Ziwa.
Pia, ameeleza kuwa mjane wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Mama Janeth Magufuli, ameahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Dkt. Samia, huku akisisitiza kuwa familia ya hayati Dkt. Magufuli itaendelea kumuombea kura kupitia kwa wananchi wa Chato na mkoa wa Geita kwa ujumla.





