Jesh la Madagascar limechukua madaraka baada ya Rais Andry Rajoelina kukimbia. Hatua hiyo inafuatia wiki kadhaa za maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana waliopinga umaskini, rushwa na ukosefu wa huduma za msingi.
Jeshi la Madagascar limechukua madaraka kutoka kwa serikali ya kiraia baada ya Rais Andry Rajoelina kukimbia nchi, hatua iliyotangazwa na kamanda wa juu wa jeshi Kanali Michael Randrianirina mjini Antananarivo.
Rajoelina, ambaye awali aliingia madarakani mwaka 2009 kupitia mapinduzi yaliyoungwa mkono na jeshi, ameng’olewa madarakani baada ya wiki kadhaa za maandamano makubwa ya vijana waliopinga umaskini, kukatika kwa huduma za umeme na maji, na rushwa serikalini.
Ofisi ya rais imelaani hatua hiyo ikiiita “uvunjaji mkubwa wa utawala wa sheria,” ikisisitiza kuwa “taifa bado limesimama.” Lakini Kanali Randrianirina alisisitiza kuwa jeshi limeamua “kubeba wajibu” na kuunda baraza la kijeshi litakalosimamia serikali ya mpito.
Harakati zilizomng’oa Rajoelina zilianza kama maandamano madogo ya vijana waliopinga kukatika kwa umeme na maji, kabla ya kugeuka kuwa vuguvugu kubwa lililoungwa mkono na vyama vya wafanyakazi na mashirika ya kiraia.
Kundi la vijana wanaojiita “Gen Z Madagascar” limekuwa kiini cha maandamano hayo, likiiga mavuguvugu kama hayo yaliozitikisa Nepal na Sri Lanka. Umoja wa Mataifa umesema takriban watu 22 waliuawa katika ukandamizaji wa awali uliofanywa na vikosi vya usalama, ingawa serikali ilipinga idadi hiyo.
