Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
KILA ifikapo Mei 23 kila mwaka huadhimishwa Siku ya Kimataifa ya Kasa, Kasa ni mnyama wa majini ambaye wengi humfananisha na kobe kwa sababu ya ufanano wao wa zaidi ya asilimia 90. Kasa ni mnyama mkongwe ambaye anasemekana kuwepo duniani kwa zaidi ya miaka millioni mia.
Kasa ni mnyama wa majini ambaye hutaga mayai yake ardhini na ana tabia ya kuyafukia mayai yake kwa mchanga ufukweni.Licha ya kuishi kwa zaidi ya miaka milioni 100, kasa wa baharini sasa wanakabiliwa na vitisho kutokana na shughuli za binadamu.
Hatari kuu ni uwindaji haramu na ulaji wa nyama ya kasa, hasa katika jamii za pwani za Tanzania na Zanzibar ambako vitendo hivi vinaendelea licha ya kuwa kinyume cha sheria. Uwindaji na biashara ya kasa wa baharini na mayai yao ulipigwa marufuku nchini na kuwepo kwa adhabu kali.
Watu wengi huamini kuwa nyama na mayai ya kasa wa baharini yana uwezo wa kutibu maradhi au kuongeza nguvu za tendo la ndoa. Hata hivyo, imani hizi huja kwa gharama ya uhai. Ulaji wa nyama ya kasa hauwapelekei tu kasa kwenye hatari ya kutoweka bali pia huweka maisha ya binadamu hatarini.
Katika tukio la kusikitisha la Machi 2024, watoto wanane na mtu mzima mmoja walifariki baada ya kula nyama ya kasa kisiwani Pemba, Zanzibar. Wengine 78 walilazwa hospitalini.
Pia mwaka 2021, watu saba, wakiwemo mtoto wa miaka mitatu, walifariki Pemba baada ya kula nyama ya kasa yenye sumu.
Katika kuhakikisha kuwa kasa wanaendelea kulindwa,Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na wadau wa mazingira na uhifadhi wamekuwa wakifanya jitihada za kutoa elimu kwa jamii ili kupunguza kasi ya kuvuliwa kwa kasa.
John Chikomo ni Mkurugenzi wa JET, anasema kuwa jitihada za kumlinda kasa zinazofanyika ni kuelimisha jamii juu ya faida za uhifadhi wa bahari na viumbe vyake akiwemo kasa ambaye kumekuwa na tishio la kutoweka kwake.
” Tunashirikiana na wadau katika kutoa elimu ya uhifadhi wa bahari na viumbe vyake ambapo kutokana na shughuli haramu za kibinadamu ndani ya bahari na imani potovu ya matumizi ya kasa na kugeuza chakula, bado jamii inahitaji uelewa mpana zaidi wa kumlinda kasa ambaye ameonyesha kutoweka.” anasema Chikomo.
Kati ya majukumu makubwa ya JET katika kuhakikisha elimu ya uhifadhi wa viumbe bahari hao inafika kwa jamii kwa uharaka na lugha rahisi, imekuwa ikitoa habari na makala mbalimbali kwenye vyombo vya Habari kupitia wanachama wake namna ya kuelimisha jamii juu kumlinda kasa na kuachana na imani potofu.
Katika kuhakikisha kuwa elimu inawafikia wananchi hasa maeneo ya wambao, JET mwaka 2018 ilishiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Kasa Duniani yaliyofanyika jijini Tanga katika Kijiji cha Chongoleani.
“Sisi kama JET tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii kupitia Habari na Makala mbalimbali zinazoandikwa na wanachama wa JET ambapo baada ya maadhimisho hayo Makala zaidi ya 25 ziliandikwa na kutoka kwenye magazeti, redio na vituo vya televisheni na kwenye mitandao ya kijamii” anasema Chikomo.
Kasa ambao wanalindwa kwa mujibu wa sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 na Kanuni za uvuvi za mwaka 2019, JET pia ilitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuandika habari za uhifadhi wa kasa zaidi ya waandishi wa habari na wahariri 110 kwa nchi nzima.
Tanzania ambayo inazo aina tano kati ya saba za kasa wa baharini wanaopatikana duniani kote ni miongoni mwa mataifa yaliyoipa nafasi siku hiyo ili kuhakikisha Kasa wanalindwa.
Aina hizo tano za Kasa hupatikana katika mwambao wa Tanzania na zote zimetajwa kuwa katika hatari ya kutoweka.
Ujumbe wa mwaka huu unasisitiza kuwalinda Kasa wa baharini kuwa ni suala la uhai kwao na kwetu.Licha ya kuishi kwa zaidi ya miaka milioni 100, kwa sasa Kasa wanakabiliwa na vitisho vikubwa vinavyosababishwa na shughuli za binadamu.
Uwindaji haramu na ulaji wa nyama ya kasa, hasa katika jamii za pwani za Tanzania na Zanzibar, bado unaendelea kuwa tishio licha ya kupigwa marufuku kisheria.
Pamoja na uvuvi haramu, lakini pia uharibifu wa fukwe nao ni changamoto kwani husababisha Kasa kukosa maeneo ya kutagia mayai, ujenzi wa mejengo karibu na bahari unatajwa kuwa tishio zaidi.
Uharibifu wa maeneo yao ya malisho ni changamoto nyingine. Tatizo kubwa zaidi ni uchafuzi wa mazingira kwa plastiki. Kasa hukosea plastiki na kudhani ni majongoo baharini au mwani, hali inayopelekea kuziba kwa njia ya chakula na hatimaye kifo.
Hata hivyo katika ripoti ya ‘State of the World’s Sea Turtles (SWOT)’ inaweka wazi kuwa Kasa wasiopungua 1,000 hufa kila mwaka kutokana na kukwama katika plastiki hii ikiwa ni sawa na kasa mmoja katika kila saa tisa. Kasa ni muhimu kwa mifumo ya maisha ya baharini na uchumi wa pwani ya Tanzania.
Kupotea kwao kunaweza kuathiri maisha yote ya baharini. Husaidia kudumisha afya ya matumbawe na mwani, maeneo muhimu kwa samaki, kamba, jodari na kaa.
Kwa kulisha na kuchimba mashimo ya kutagia, huandaa makazi kwa viumbe wengine. Kama wawindaji na mawindo yao, wanasaidia kusawazisha mnyororo wa chakula baharini.
Ritha Johansen, mwakilishi wa Wild Africa nchini Tanzania, anasema: “Karibu vitisho vyote vinavyowakabili Kasa na makazi yao vinasababishwa na binadamu.
Ulaji wa kasa si hatari tu kwa spishi hizi zilizo hatarini, bali pia ni tishio la moja kwa moja kwa maisha ya binadamu.
“Tunahitaji kubadili mitazamo na tabia kuhusu uwindaji haramu na ulaji wa kasa kwa faida ya viumbe hawa na jamii zinazowazunguka. Uwindaji unatuibia sote. Tukiwapoteza kasa, tunapoteza sehemu muhimu ya mfumo wa bahari. Kuwalinda ni kulinda mazingira ya baharini, urithi wetu wa kitamaduni, na vizazi vijavyo.” anasema.
Anasema kuwa hali ni mbaya, lakini bado kuna matumaini, mwaka jana, Serikali, wataalamu wa kisayansi na wadau wa kimataifa walikutana kwenye Mkutano wa 9 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kumbukumbu wa IOSEA na kujadliana kuhusu Kasa wa Baharini ili kuratibu juhudi za uhifadhi katika Bahari ya Hindi na Asia ya Kusini Mashariki.
Miongoni mwa matokeo ni kupitishwa kwa Mpango wa Hatua Maalum kwa aina ya kasa walioko hatarini kutoweka kabisa, ambapo walitoa mapendekezo ya usimamizi wa fukwe na taratibu za vizalia, pamoja na kupitishwa kwa mwongozo wa kutambua maeneo muhimu kwa kasa.
Katika siku ya mwisho ya mkutano huo, Nchi ya Kuwait inayohifadhi aina tano kati ya saba za kasa wa baharini — ikawa nchi ya 36 kusaini mkataba huo.
“Mapendekezo hayo anaweza kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kusema hapana kwa uwindaji haramu na ulaji wa nyama ya kasa wa baharini. Kwa pamoja, tunaweza kulinda viumbe wa baharini na jamii, na kurejesha bioanuwai ya bahari zetu kwa ajili ya vizazi vijavyo” anasema.
