Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kinawatakia heri wanawake wote nchini na duniani katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani leo Machi 8,2026.
JET inatambua mchango mkubwa wa mwanamke katika kulinda na kuhifadhi mazingira.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, imesema kwa muda mrefu wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika matumizi ya rasilimali asilia ndani ya familia na jamii, hivyo kuwa na nafasi muhimu katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mwanamke ndiye mlezi wa familia na mara nyingi ndiye anayehusika moja kwa moja na matumizi ya nishati ya kupikia, maji, na rasilimali nyingine muhimu za mazingira.
Kupitia nafasi hiyo, wanawake wameendelea kuwa kichocheo muhimu cha utunzaji wa mazingira, kwa kuhamasisha matumizi bora ya rasilimali, kupunguza uharibifu wa misitu, na kuhimiza mbinu rafiki kwa mazingira katika shughuli za kila siku za kijamii na kiuchumi.
Katika maadhimisho haya, JET pia inatoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti katika kulinda mazingira, hususan kupitia ajenda ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Hatua hii ni muhimu katika kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa, kuboresha afya za wananchi, na kuchangia juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
JET inaamini kuwa juhudi hizi zina mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo endelevu na kulinda mifumo ya ikolojia ambayo ndiyo msingi wa ustawi wa jamii na uchumi wa Taifa.
Aidha, JET inatoa wito kwa wadau wote—serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla—kuendelea kuwawezesha wanawake kwa elimu, teknolojia na rasilimali zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira.
Uwezeshaji wa wanawake katika masuala ya mazingira ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa Taifa na dunia kwa ujumla.
Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania kitaendelea kutumia taaluma ya uandishi wa habari kuelimisha umma, kuhamasisha uwajibikaji, na kukuza uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu.
John Chikomo
Kwa niaba ya
Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).




