Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete leo ameweka saini katika kitabu cha maombolezo ya kifo cha Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam marehemu Muadhama Polycarp Kardinali Pengo katika kanisa la Mtakatifu Yosefu jijini.
Dkt Kikwete baada ya kuweka saini alimpa mkono wa pole Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mhashama Thaddaeus S. Ruwa’ichi, na kusema daima marehemu Muadhama Pengo atakumbukwa kwa mchango wake adhimu na kwa moyo wake wa upendo kwa wananchi wenzake na kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba alikuwa rafiki wa wengi.
Aidha, Dkt Kikwete akitoa pole hizo kwa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki, amewataka kuwa na subira katika kipindi hiki cha majonzi huku akiungana nao kumuombea marehemu apumzike kwa amani.

Akiongea na wanahabari baada ya kutoa mkono wa pole, Rais huyo Mstaafu alisema yeye na Marehemu Muadhama Polycarp Kardinali Pengo walikuwa wanafahamiana toka siku nyingi zilizopita, hususan akiwa wilayani Nachingwea kituo chake cha kwanza cha kazi na marehemu akiwa Askofu Mkuu wa Tunduru na Lindi miaka ya 1970.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mhashama Thaddaeus S. Ruwa’ichi, akitangaza msiba huo mzito mnmo tarehe 19/02/2026 saa 04:00 alisema kwa majonzi kuwa mpendwa baba yetu Mwadhama Polycarp Cardinal Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ameitwa nyumbani kwa Baba wa Milele akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ratiba rasmi ya shughuli za mazishi zitakazofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam, pamoja na Kituo cha Hija Pugu, shughuii za kuaga mwili wa marehemu zitaanza siku ya Ijumaa tarehe 27 Februari 2026 ambapo mwili utawasili katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu saa 03:00 asubuhi chini ya uratibu wa Kamati ya Mazishi.
Kuanzia saa 03:15 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, waombolezaji watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu.
Saa 10:00 jioni kutakuwa na Misa Takatifu ya kumuombea marehemu itakayofuatiwa na mkesha wa sala na maombolezo utakaoshirikisha makundi mbalimbali ya kijimbo yakiwemo watawa, walei pamoja na vyama vya kitume.

Siku inayofuata, mwili wa marehemu utaondoka Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu saa 12:00 asubuhi kuelekea Kituo cha Hija Pugu, na unatarajiwa kuwasili saa 12:45 asubuhi chini ya usimamizi wa Kamati ya Mazishi.
Kuanzia saa 01:00 hadi saa 03:45 asubuhi waombolezaji watapata tena fursa ya kutoa heshima za mwisho katika Kituo cha Hija Pugu.
Misa ya Mazishi itaanza saa 04:00 asubuhi katika Kituo cha Hija Pugu ikihitimisha rasmi shughuli za mazishi Jumamosi.
Waumini na wananchi wote wanaombwa kushiriki katika ibada na sala hizi kwa utulivu na heshima inayostahili.
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alizaliwa tarehe 5 Agosti 1944 na kupadrishwa mwaka 1971. Alisoma Teolojia ya Maadili katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, Roma, na kupata shahada ya uzamivu mwaka 1977. Aliwahi kufundisha katika Seminari ya Kipalapala na kuwa Rektor wa kwanza wa Seminari ya Segerea hadi 1983.
Aliteuliwa kuwa Askofu wa Nachingwea mwaka 1983 na baadaye Tunduru–Masasi mwaka 1985. Mwaka 1990 akawa Askofu Mkuu Msaidizi wa Dar es Salaam, na mwaka 1992 akawa Askofu Mkuu kamili. Alitangazwa kuwa Kardinali mwaka 1998 na Papa Yohane Paulo II, na alishiriki katika mikutano ya kumchagua Papa mwaka 2005 na 2013.
Alihudumu katika idara mbalimbali za Kanisa la Roma na kuongoza SECAM tangu 2007. Alistaafu mwaka 2019, akiacha alama ya uongozi thabiti na imani isiyotetereka.




