Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na kampuni ya ABC Group inayojuhusisha na usambazaji wa vifaa vya ujenzi kufikisha huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo kwa wananchi.

Ushirikiano huo utafanyika kupitia wateja watakaonunua vifaa vya ujenzi katika kampuni ya ABC Group kupewa vocha yenye punguzo la asilimia 20 kupata huduma za matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza adhma yake ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo kwa urahisi zaidi.

“Kupitia ushirikiano huu wateja watakaonunua vifaa vya ujenzi katika kampuni ya ABC Group watapata punguzo la asilimia 20 kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo na kuongezewa uelewa kuhusu magonjwa hayo”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema ushirikiano huo pia utawahusisha wagonjwa wanaopata huduma katika Taasisi hiyo kupatiwa punguzo maalumu la bei watakapoenda kununua vifaa vya ujenzi katika kampuni ya ABC Group.

Aidha Dkt. kisenge alitoa wito kwa makampuni na Taasisi nyingine kuungana na JKCI katika juhudi za kuielimisha jamii kuhusu kinga na matibabu ya magonjwa ya moyo kama alivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya ABC Group Mohammad Shareef aliushukuru uongozi wa JKCI kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo na kuishirikisha katika masuala ya kufikisha huduma za afya katika jamii.

“Tutashirikian na JKCI kujenga uelewa kwa jamii kuhusu afya ya moyo pamoja na umuhimu wa kuwa na mazingira bora ya makazi, tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zitakazotolewa na JKCI na jinsi zitakavyoweza kuwanufaisha”, alisema Shareef

Ushirikiano kati ya JKCI na kampuni ya ABC Group unatarajiwa kuongeza mwamko wa jamii kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuchukua hatua za mapema dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya ABC Group Mohammed Shareef mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kusaini mkataba  wa ushirikiano kati ya Taasisi hizo kuwatibu wateja wa ABC kwa punguzo la asilimia 20 iliyofanyika leo katika ofisi za ABC zilizopo jijini Dar es Salaam.  Picha na JKCI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya ABC Group Mohammed Shareef wakisaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kuwatibu wateja wa ABC Group Tanzania kwa punguzo la asilimia 20, uliofanyika katika ofisi za ABC jijini leo Dar es Salaam.  
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiongea na waandishi wa habari wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano kati ya JKCI na Kampuni ya ABC Group kuwatibu wateja wa ABC kwa punguzo la asilimia 20 iliyofanyika leo katika ofisi za ABC zilizopo jijini Dar es Salaam.