Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Burkina Faso wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi ya matibabu ya  magonjwa ya moyo.

Hati hizo zimesainiwa jana jijini Dar es Salaam kati ya  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo Dkt. Kisenge alisema makubaliano hayo yataimarisha utoaji wa  huduma za matibabu ya moyo nchini Burkina Faso na kuokoa maisha ya wananchi wenye matatizo ya moyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore wakibadilishana hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi za matibabu ya moyo jana jijini Dar es Salaam.

“Tumekubaliana kuwasaidia katika kufanya tatifi, kuwafundisha  wataalamu wa afya wakiwemo madaktari, wauguzi na wataalamu wa vifaa tiba jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo na namna ya kutumia vifaa tiba vya moyo pia watawatuma wagonjwa ambao wameshindwa kuwafanyia upasuaji waje kutibiwa katika taasisi yetu”.

Katika kutoa mafunzo ya kuwatibu wagonjwa ya moyo kuna wataalamu wetu ambao watakwenda Burkina Faso kufundisha na kuna wataalamu kutoka nchini humo watakaokuja  kujifunza katika taasisi yetu”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kuhusiana na upatikanaji wa vifaa tiba wamekubaliana wanunue katika  Bohari ya Dawa (MSD) ambao ni wasambazaji wa vifaa hivyo katika taasisi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi za matibabu  ya moyo jana jijini Dar es Salaam.

“Kwa namna ya kipekee namshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha tiba ya magonjwa ya moyo katika taasisi yetu  kitu ambacho kimesababisha nchi mbalimbali kuja  kujifunza namna ya kutoa matibabu ya moyo katika nchi zao pia kuwaleta wagonjwa wao kutibiwa JKCI”.

“Pia ninamshukuru Rais wa Bukina Faso Mhe. Kapteni Ibrahimu Traore kwa kuiamini nchi yetu na kuwatuma wataalamu wake ambao tumesaini makubaliano nao ili nao kupitia sisi wawe taasisi bora ya matibabu ya moyo na kufika hatua tuliyoifikia sisi na leo tumeingia katika historia na Burkina Faso ya kutangaza utalii tiba ambao umekuja katika afya”, alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais,  Drissa Traore ambaye kwa mara ya pili ameongoza timu hiyo ya wataalamu kuja hapa nchini alisema siku ya kwanza walipotembelea JKCI walivutiwa kwa huduma wanazozitoa pamoja na uhusiano mzuri wa uongozi wa manejimenti uliokuwepo baada ya kurudi nchini kwao walivichukuwa hivyo vyote na kuvifanyia kazi.

“Ninawashukuru maraisi wetu wa Burkina Faso Mhe. Kapteni Ibrahimu Traore na wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa tayari kuimarisha huduma za afya katika nchi zao, nimevutiwa na JKCI kwani haitoi huduma tu Tanzania bali Afrika nzima  ndiyo maana nasi tumekuja kujifunza. Tunawategemea sana katika mafunzo, tafiti na matibabu ya moyo kwa afya za watu wa Burkina Faso”, alisema Traore.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore waonesha hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi za matibabu ya moyo mara baada ya kuisaini jana jijini Dar es Salaam.

Mapema mwezi wa pili mwaka huu Rais wa Burkina Faso Mhe. Kapteni Ibrahimu Traore alituma timu ya wataalamu kwenda kujifunza katika taasisi hiyo na kuona  hatua walizopitia katika tiba ya moyo hadi kuwa moja ya Taasisi zinazoongoza Barani Afrika kutoa huduma za kibingwa bobezi ili nao waweze kujifunza na kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini humo.

Utiaji saini wa makubaliano hayo ni jitihada zilizofanywa na ubalozi wa Tanzania nchini Burkina Faso unaowakilisha nchi hiyo kutokea Abuja, Nigeria unaoongozwa na Mhe. Balozi Selestine Kakele ambao waliratibu mawasiliano ya JKCI na Burkina Faso na kuhakikisha yanafanyika na hatimaye kufanikisha kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya ushirikiano huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore, viongozi wa JKCI na wataalamu kutoka Burkina Faso mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi za matibabu ya moyo iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.