Na Jeremiah Ombelo
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeelezea inavyotumia teknolojia ya tiba mtandao (Telehealth) katika kuboresha huduma za afya inazozitoa kumsaidia mgonjwa kuwasiliana na daktari popote alipo.
Hayo yameeleza na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya wakati wa Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililokuwa likifanyika katika kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salaam na kumalizika hivi karibuni.
Taasisi hiyo pia imeeleza jinsi inavyotumia teknolojia kwa kutumia kifaa kijulikanacho kwa jina la Dozee kufuatilia hali ya mgonjwa akiwa nyumbani kwa kufuatilia mzunguko wa damu, shinikizo la damu na mapigo ya moyo.

“Tupo katika kongamano hili la kisayansi kuwapa elimu wadau wa afya namna ambavyo JKCI inatumia teknolojia katika masuala ya Tiba mtandao (Telehealth) na huduma za kuchunguza hali ya mgonjwa aliyopo nyumbani kwa kutumia kifaa cha Dozee”, alisema Dkt. Angela.
Dkt. Angela alisema katika kongamano hilo wataalamu wa afya wameweza kujadili mada mbalimbali ikiwemo machapisho na tafiti zilizofanywa na wataalamu wa JKCI kupitia MUHAS ambazo zimetoa matokeo yenye mchango mkubwa uliofanyika katika sekta ya afya.
“Moja ya mafanikio makubwa yaliyojadiliwa kwenye kongamano hilo ni pamoja na uzinduzi rasmi wa Kituo cha Taifa cha Tafiti na Matibabu ya Mishipa ya Damu na Magonjwa ya Moyo (Centre of Excellence for East and Central Africa)”,
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango mkubwa alioufanya katika kufanikisha uanzishwaji wa kituo hiki muhimu cha Tafiti na Matibabu ya Mishipa ya Damu na Magonjwa ya Moyo (Centre of Excellence for East and Central Africa)” alisema Dkt. Muhozya.

Kwa upande wake Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli Msigwa alieleza kuwa JKCI ina teknolojia zinazoweza kuokoa maisha pale ambapo mgonjwa anakuwa kwenye hali inahohitaji huduma ya dharura na haraka.
“Tunatumia teknolojia kutoa huduma kwa wagonjwa wetu ambapo kwa kutumia kifaa cha Dozee kinachotuwezesha kutoa huduma ya haraka na kuokoa maisha ya mgonjwa pale inapotuonyesha mzunguko wa damu ya mgonjwa, shinikizo la damu na mapigo ya moyo ya mgonjwa haviko sawa,”
“Upande wa huduma ya Telehealth wagonjwa wetu wanaweza kuzungumza na dakatari kwa njia ya mtandao, kupata ushauri wa kitaalamu, kuandikiwa vipimo na dawa bila kufika hospitalini kwani kinachohitajika kufanikisha huduma hii ni simu janja ama kompyuta kwaajili ya kuweka miadi na kuonana na daktari mtandaoni”, alisema Dkt. Msigwa.
