Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Shinyanga
Changamoto ya kiuchumi kwa jamii imekuwa ni kikwazo kwa baadhi watoto kuendelea na matibabu ya moyo hali iliyosababisha kuchelewa kupata matibabu ambayo yangeokoa maisha yao.
Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nuru Letara wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kambi maalum ya matibabu ya moyo yanayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH).
Dkt. Nuru alisema wazazi na walezi wengi wanakutana na changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazopelekea kushindwa kuwapeleka watoto wao hospitali kupata matibabu.
“Changamoto zipo nyingi ila changamoto kubwa ni hali duni ya uchumi ambayo inasababisha wazazi na walezi kukosa nauli vilevile kukosa pesa ya kulipia gharama za matibabu, lakini tunapokutana nao tunawatia moyo na kuwasaodia”, alisema Dkt. Nuru.
Dkt. Nuru alisema miongoni mwa wagonjwa waliopewa rufaa katika kambi hiyo ni mtoto aliyegendulika kuwa na tatizo la moyo kwenye kambi ya matibabu ya moyo iliyofanywa na wataalamu wa JKCI mwaka mmoja uliopita lakini hakuweza kwenda kufanyiwa upasuaji kutokana na changamoto za kifedha.
“Katika kambi hii tumempa dawa za awali za kutumia pia tumempa barua ya rufaa ya kuja kutibiwa JKCI. Kila kitu kikienda sawa atafanyiwa upasuaji wa ,oyo mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu katika kambi maalumu ya madaktari kutoka nchini Saudi Arabia”, alisema Dkt. Nuru.

Dkt. Nuru pia aliwaomba wazazi kujua afya za watoto wao kwa kujua dalili za magonjwa ya moyo ili waweze kupata matibabu mapema.
“Watoto wengine hupata shida ya kupumua, hukosa nguvu ya kunyonya, hutokwa jasho wakiwa wananyonya na wakati mwingine ngozi hubadilika rangi na kuonekana ya bluu, dalili hizi zikionekana mapema zinahitaji kuchunguzwa hospitalini ili kuokoa maisha yao”, alisema Dkt. Nuru.
Kwa upande wake Bibi wa mtoto mwenye tatizo la moyo Monica Stephano mkazi wa Ushetu alisema waligundua hali hiyo mtoto akiwa na umri wa miezi sita lakini walishindwa kuendelea na matibabu kutokana na gharama kubwa walizoshindwa kuzimudu.
“Tulifurahi kusikia kwamba madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wanakuja Shinyanga, tumepata matumaini mapya na tunashukuru kwamba sasa mjukuu wangu ana nafasi ya kufanyiwa upasuaji kwa kusaidiwa kulipiwa matibabu hayo”.
“Tumefika hapa mtoto amepimwa lakini tundu kwenye moyo wake bado lipo na anatakiwa kufanyiwa upasuaji, nimefurahi
sana na Mungu awazidishie pale walipotoa wote waliochangia matibabu ya moyo kwa watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchuni”, alisema Bibi Monica.

Naye mkazi wa Kishapu Lucas Marwa ambaye mtoto wake alipata huduma katika kambi hiyo alisema changamoto walizokuwa wakizipitia ni kutokupata majibu sahihi kila walipokwenda hospitalini, lakini sasa wamepata majibu mazuri na mwelekeo wa matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
“Madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametupa mwanga mpya, tunaomba wadau mbalimbali waendelee kusaidia huduma hizi kwani zinagusa maisha ya familia nyingi”, alisema Marwa.
