Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanza mchakato wa kuanzisha huduma ya upandikizaji wa moyo inayotarajiwa kukamilika baada ya miaka mitano na kuanza kutoa huduma hiyo.

Kukamilika kwa mchakato huo kunatarajiwa kuendelea kuiweka Tanzania kwenye ramani ya nchi inayotoa huduma za juu za matibabu ya moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema mchakato huo ni wakihistoria na utafungua ukurasa mpya katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini. 

Dkt. Kisenge alisema katika kuelekea maadhimisho ya Miaka 10 ya JKCI taasisi hiyo imeona ianze kuweka mikakati ya kutoa huduma ya kupandikiza moyo kwani ni huduma ambayo imekuwa ikitafutwa na wagonjwa wengi wa moyo katika bara la Afrika.

“Tayari tumezindua Kamati maalum ya upandikizaji wa moyo itakayosimamia maandalizi yote ya kitaalamu, kisheria na kiutendaji ndani ya kipindi cha miaka mitano. Hii ni hatua kubwa kwa nchi yetu na pia kwa nchi jirani ambazo hazina huduma hii,” alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema huduma hiyo ya upandikizaji wa moyo ina mchakato wa muda mrefu na maandalizi yakutosha katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji wa vifaa tiba vya kisasa, mafunzo ya wataalamu, pamoja na utaratibu wa kisheria na kimaadili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Upandikizaji wa Moyo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Evarist Nyawawa alisema utekelezaji wa mpango huo utafuata mifumo bora ya utoaji wa huduma hiyo kukidhi viwango vya kimataifa.

Dkt. Nyawawa ambaye pia ni bingwa wa upasuaji wa moyo katika Taasisi hiyo alisema takwimu zinaonesha watu zaidi ya 50,000 duniani wameshafanyiwa upandikizaji wa moyo na umekuwa wa mafanikio hivyo hata JKCI itaweza kutoa huduma hiyo.

Mpango huo ni sehemu ya jitihada za JKCI katika kuimarisha huduma za kitaifa na kimataifa za moyo kupunguza rufaa za nje ya nchi na kuifanya taasisi hiyo kuwa kitovu cha huduma za moyo ukanda ya Afrika Mashariki na kati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwajulia hali wanachama wa chama cha wagonjwa wa moyo Tanzania wakati wa uzinduzi wa kamati ya upandikizaji moyo uliofanyika leo katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi mfano wa moyo Mwenyekiti wa kamati ya upandikizaji moyo Dkt. Everist Nyawawa wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo leo katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanachama wa chama cha wagonjwa wa moyo Tanzania wakisikiliza wakati wa uzinduzi wa kamati ya upandikizaji moyo uliofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) uliopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na wahariri wa vyombo vya habari mara baada kumalizika kwa uzinduzi wa kamati ya upandikizaji moyo leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. (Picha na: JKCI)