Na Mwandishi Maalum

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kusogeza huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa jamii kwa kuwalenga wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi hatua inayolenga kuwafikia wale ambao mara nyingi hukosa muda wa kufuatilia afya zao kutokana na majukumu ya kazi.

Huduma hizo hutolewa moja kwa moja katika kampuni, mashirika ya serikali na taasisi binafsi ambapo wafanyakazi hufanyiwa uchunguzi wa afya, matibabu pamoja na elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nyanjura Nyaruga akimpima kiwango cha sukari kwenye damu Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA) Charles Shirima wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo iliyofanyika katika ofisi za CMSA zilizopo Garden Avenue Tower jijini Dar es Salaam.

Akitoa elimu ya magonjwa ya moyo hivi karibuni kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Daktari Bingwa wa JKCI, Theophil Mushi alisema taasisi hiyo imepanua wigo wa utoaji wa huduma ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa bila kuathiri muda wao wa kazi.

“Tumesogeza huduma na sasa tunawafuata wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi. Tunawafanyia uchunguzi, kutoa matibabu na kuwapa elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Theophil.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA. Nicodemas Mkama, aliipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa hatua hiyo, akisema imewasaidia wafanyakazi kupata huduma bila kupoteza muda wa kazi.

“JKCI imefanya uamuzi mzuri kutufikia na kutupa huduma hizi muhimu. Wafanyakazi wetu wameweza kuchunguza afya zao bila kuathiri muda wao wa kazi”, alisema CPA. Mkama.

Aliongeza kuwa baada ya huduma hizo, wafanyakazi wa CMSA sasa wana uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kufuatilia afya zao na wanaweza kuendelea kupata huduma katika matawi ya JKCI ya Oysterbay na Kawe Kliniki.

Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Maria Samlongo akitoa elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa moyo kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA) wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo iliyofanyika katika ofisi zao zilizopo Garden Avenue Tower jijini Dar es Salaam.

Naye Afisa Lishe wa JKCI, Maria Samlongo alisema taasisi hiyo imetoa elimu ya lishe kwa wafanyakazi wa CMSA ili kuwasaidia kuchagua vyakula bora na kuelewa madhara ya mifumo isiyo sahihi ya maisha.

“Kupitia huduma hizi tumetoa ushauri wa mtu mmoja mmoja kuhusu umuhimu wa lishe bora katika kujenga afya ya moyo. Uelewa wa jamii kuhusu makundi sahihi ya chakula bado ni mdogo, ndiyo maana JKCI tumekuwa tukiwafuata wananchi kule waliko ili kuwajengea uelewa wa pamoja”, alisema Maria.

Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wafanyakazi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kambi maalumu ya uchunguzi