Na: Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Kwa mara ya kwanza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) yawekea historia Tanzania, Afrika Mashariki na Kati kwa kutoa matibabu mapya ya tiba ya kupunguza msisimko wa shinikizo la damu katika mishipa ya figo (Renal denervation therapy).
Matibabu hayo ambayo yameanza kutolewa leo katika Taasisi hiyo yanatolewa kwa wagonjwa wenye matatizo ya shinikizo la juu la damu la muda mrefu ambalo halishuki kwa matibabu ya dawa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema yatizo la shinikizo la juu la damu huchangia kwa asilima 25 ya magonjwa yote yasiyoambukiza hivyo kupelekea vifo vingi vya ghafla na kuongeza idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya kusafishwa damu (dialysis).
“Matibabu haya hutibiwa kwa kutumia mashine ya radio frequency ultrasound ambayo inaenda kuchoma mishipa inayoenda kwenye figo ili kuweza kupunguza tatizo la shinikizo la juu la damu na kuwa la dawaida”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema kupitia matibabu hayo wagonjwa wenye matatizo ya shinikizo la juu la damu la muda mrefu wanapunguziwa hatari ya kupata kiharusi, magonjwa ya figo kutofanya kazi vizuri lakini pia inasaidia kudhibiti uzalishaji wa homoni zinazopandisha shinikizo la damu.
“Matibabu haya ni ya gharama sana, mgonjwa mmoja inaweza mgharimu kiasi cha shilingi milioni 22 kupata huduma hii lakini kupitia Serikali yetu wagonjwa wanaopata huduma hii leo watatibiwa kwa kuchangia kidogo na wale wasiokuwa na uwezo watatibiwa bila gharama”, alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri Prof. Mohamed Atef alisema matibabu hayo yanatoa matumaini kwa wagonjwa wenye matatizo ya shinikizo la damu la juu ambao wamekuwa wakitumia dawa kwa muda mrefu bila ya mafanikio.
“Leo tutawapatia matibabu wagonjwa sita hadi saba wenye matatizo ya shinikizo la juu la damu la muda mrefu kwa kufanyiwa upasuaji mdogo kupitia tundu dogo lililopo kwenye paja na kuunguza mishipa ya damu inayoelekea kwenye figo na kusababisha matatizo ya figo”, alisema Dkt. Atef.

Dkt. Atef alisema Tanzania inapaswa kujivunia kwa kuwa na Taasisi ya Moyo nchini ambayo inatoa matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo na kuongeza ujuzi katika kutoa matibabu hayo.
“Ninafura kwa kuwa daktari wakwaza kufikisha ujuzi huu hapa JKCI, naupongeza sana uongozi wa hapa kwa kuhakikisha ndoto ya kufikisha matibabu bingwa na mbinu mpya kwa wagonjwa wake inatimia”, alisema Dkt. Atef
Naye mgonjwa aliyekuwa akisubiri kupatiwa matibabu hayo Donasian Meleki aliushukuru uongozi wa JKCI kwa kumruhusu kuchangia kidogo matibabu hayo na gharama zilizobaki kulipwa na Serikali.
Meleki alisema ugonjwa wa shinikizo la damu amekuwa nao tangu mwaka 2011 ambao umemsababishia kupata matatizo ya figo na kufikia hatua ya kusafisha damu (dialysis).
“Naishukuru Serikali ya Tanzania kwa kujali afya za watu wake, hapa ndio naenda kufanyiwa upasuaji ninaimani nitatoka salama na kupunguza matatizo yaliyopo katika mwili wangu hivyo kuendelea kulitumikia Taifa”, alisema Meleki
Matibabu ya tiba ya kupunguza msisimko wa shinikizo la damu katika mishipa ya figo (Renal denervation therapy) yalianza kutolewa duniani mwaka 2013 lakini hayakuwa na mafanikio mazuri hivyo kufanyiwa utafiti ambao sasa umeonesha mafaniko na kuanza kutolewa tena kwa wagonjwa wenye matatizo ya shinikizo la juu la damu la muda mrefu ambalo halishuki kwa kutumia dawa.
