Mgogoro wa Ukraine unaendelea kuingia katika hatua ngumu, huku mashambulizi ya kijeshi yakiendelea kuathiri maisha ya raia.

Wakati juhudi za kidiplomasia, misaada ya kimataifa, na msukumo wa vikwazo dhidi ya Urusi vikiendelea kuongezeka, mataifa mbalimbali yanaonesha dhamira ya kuisaidia Ukraine kijeshi na kiuchumi, huku hali ya usalama, misaada ya kibinadamu na nafasi ya suluhu ya amani vikiwa bado ni masuala yenye mvutano mkubwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov na mwenzake wa Marekani Marco Rubio walikutana kwa mazungumzo katika mji mkuu wa Malaysia wa Kuala Lumpur kando ya mkutano wa ASEAN na kujadili kuhusu vita vya Ukraine lakini kulikuwa na matarajio hafifu ya kufikia mafanikio yoyote.

Viongozi hao walikutana saa chache baada ya Moscow kuushambulia vikali mji mkuu wa Ukraine Kyiv kwa usiku wa pili mfululizo huku Umoja wa Mataifa ukitahadharisha kuwa idadi ya wahanga wa mashambulizi ya Urusi imefikia kiwango cha juu zaidi.