Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali imesema jukumu la kuwapandisha vyeo watumishi ni la mwajiri husika.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Alice Kaijage aliyetaka kufahamu mpango wa serikali kuhakikisha kada nyingine wanapewa Madaraja ya Mserereko kama ilivyo kwa Kada ya Ualimu.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 6 (1) (b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura, 298 jukumu la kuwapandisha vyeo watumishi ni la Mwajiri husika.

“Jukumu hili hutekekelezwa baada ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutoa mwongozo kuwataka waajiri kuandaa na kuwasilisha Ikama na Bajeti ya Mwaka husika wa fedha na Ofisi kuridhia utekekelezaji wa bajeti hiyo,” amesema.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali iliwapandisha vyeo kwa mserereko watumishi wasio walimu 1,284.

“Aidha, Kwa mwaka 2024/2025, Serikali imetoa Mwongozo unaohusu upandishaji vyeo na ubadilishaji kada ikiwemo na kwa watumishi waliocheleweshwa kupandishwa vyeo.

“Hivyo, nitoe wito kwa waajiri wote katika Sekta ya Umma kutekeleza kwa wakati mwongozo huo ili kuepusha malalamiko kwa watumishi wa Umma wenye changamoto za kupandishwa vyeo,” amesema.