Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, amesema hakuna nguvu itakayoweza kuizuia ACT kutoshinda Urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, hata kama uchaguzi huo ungefanyika kwa mwezi mzima na sio kwa siku mbili pekee.

Akizungumza katika uzinduzi wa timu za ushindi uliofanyika katika ukumbi wa Majid Hall, Kiembe Samaki, Babu Duni alisema wananchi wameshachoka na mfumo wa sasa, na sasa sauti ya mabadiliko imesikika kila kona ya visiwa vya Zanzibar.

Alisema ACT Wazalendo kimepitia changamoto kubwa ikiwemo kifo cha Almarhum Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na uporaji wa uchaguzi wa mwaka 2020, lakini chama hakikurudi nyuma.

Ameeleza kuwa kila siku wananchi wamezidi kukiamini kutokana na dhamira ya kweli walionayo ya kuikomboa Zanzibar.

Kwa upande wake, Meneja wa kampeni za Mgombea Urais, Ismail Jussa Ladhu, alisema uzinduzi wa kamati hizo za ushindi ni sehemu ya mkakati wa ACT kushika nafasi ya urais.

Alibainisha kuwa viongozi wa chama katika ngazi za mikoa na majimbo wana hamasa kubwa ya kufanya kazi za chama, na ari hiyo ndiyo ishara ya ushindi mkubwa utakaopatikana ifikapo Oktoba 29.

Jussa aliongeza kuwa ushindi wa awamu hii utakuwa mkubwa zaidi kwa sababu idadi kubwa ya wanachama na hata viongozi wa CCM wamekimbia chama hicho kutokana na kuchoshwa na hali ya sasa.

Alisema mgombea wa CCM ameshindwa kuwaamini wananchi wa Zanzibar, jambo ambalo limezua hasira za kimya zitakazodhihirika kwenye sanduku la kura.

“Hii ndio sehemu ambayo amemuondoa kwenye mapenzi na watu wa kisiwa hiki. Asione wamenyamaza kimya, watu watamuonesha kwenye sanduku la kura,” alisema Jussa.

Babu Duni alihitimisha hotuba yake kwa kusema matatizo ya njaa na umasikini hayawatambui wanachama wa chama fulani bali yanawakumba Wazanzibari wote.

Alisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kusimama imara na kumchagua Othman Masoud na ACT Wazalendo kwa ajili ya Zanzibar mpya yenye heshima, maendeleo na uhuru wa kweli.