Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
JUMLA ya watahiniwa 134,390 wamesajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Sita 2025 unaoanza kesho ambapo watahiniwa wa shule ni 126,957 na watahiniwa wa kujitegemea ni 7,433.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 04, 2025, Katibu Mtendaji wa wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dkt. Said Mohamed amesema kati ya watahiniwa wa shule 126,957 waliosajiliwa wavulana ni 64,581 sawa na asilimia 50.87 na wasichana ni 62,376 sawa na asilimia 49.13.

Amefafanua kuwa, watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 453 ambapo kati yao wenye uoni hafifu ni 300, wasioona ni 16, wenye uziwi 58, wenye ulemavu wa akili 04 na wenye ulemavu wa viungo vya mwili ni 75.
“Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 7,433 waliosajiliwa, wavulana ni 4,782 sawa na asilimia 64.33 na wasichana ni 2,651 sawa na asilimia 35.67. Aidha, watahiniwa wa kujitegemea wenye mahitaji maalum wako 151 ambapo kati yao wenye uoni hafifu ni 142 na wasioona ni 9,” amesema.
Ameongeza kuwa mwaka 2024 idadi ya watahiniwa wa Shule na kujitegemea waliosajiliwa walikuwa 113,536, hivyo ongezeko la jumla ya watahiniwa 20,854 ambayo ni sawa na asilimia 18.37 kwa mwaka 2025.
Aidha amesema kuwa jumla ya watahiniwa 10,895 wamesajiliwa kufanya Mtihani wa Ualimu ambapo kati ya hao 3,100 ni wa ngazi ya Stashahada na 7,795 ni wa ngazi ya cheti.
Amesema watahiniwa wenye mahitaji maalum waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Ualimu ni 23, kati yao wenye uoni hafifu kwa ngazi ya Stashahada na 16 wenye uoni hafifu, 3 wasioona, 1 uziwi, 1 ulemavu wa viungo ni wa ngazi ya cheti.
“Maandalizi yote yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa Mitihani husika, vijitabu vya kujibiwa na nyaraka zote muhimu zinazowahusu mitihani hiyo katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.
“Pamoja na maandalizi yote muhimu yaliyofanyika, Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri zihakikishe kuwa Usalama wa vituo unaimarishwa na kwamba vituo hivyo vinatumika kwa mujibu wa Mwongozo uliotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania,” amesisisitiza.
Hata hivyo Baraza limetoa wito kwa watahiniwa hao, kutokujihisisha na vitendo vya udanganyifu na yeyote atakayebainika matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani.
“Baraza linawaasa wakuu wa Shule na wakuu wa vyuo kutekeleza majukumu yao ya usimamizi kwa kuzingatia Mwongozo wa Usimamizi uliotolewa. Pia Baraza linatoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote asiyehusika na Mitihani anaingia kwenye maeneo ya shule na vyuoni,” amesema.