Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila amesema anapanga hivi karibuni kutembelea mji wa Goma uliodhibitiwa na waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wa M23.

Kabila aliitaja serikali ya sasa ya Kongo kuwa ya kidikteta baada ya bunge kumuondolea kinga na kufungua njia ya kiongozi huyo wa zamani aliye na miaka 53 kushitakiwa dhidi ya tuhuma za uhalifu wa kivita, uhaini na kushiriki katika harakati za uasi.

Katika hotuba yake iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii, Kabila aliyeiongoza Kongo kuanzia mwaka 2001 hadi 2019 amemlaumu rais wa sasa Felix Tshisekedi ambaye awali alidai Kabila anashirikiana na waasi wa M23.

Kabila alisema kutokana na fununu za kwamba tayari ameutemebela mji wa Goma serikali ya Kongo ikachukua uamuzi wa kiholela wa kumuondolea kinga.

“Siku chache zilizopita kufuatia uvumi kutoka mitaani au mitandaoni kuhusu madai ya kuwepo kwangu Goma, ambako nitaenda katika siku zijazo, kama ilivyotangazwa, utawala mjini Kinshasa ulichukua maamuzi ya kiholela ya kizembe bila kufikiria, na hii inaonesha kupungua kwa demokrasia nchini humo,”alisema Kabila

Katika hotuba yake hiyo Joseh kabila alisema ni lazima udikteta ukomeshwe Kongo. Akisistiza kwamba demokrasia, hali nzuri ya uchumi na utawala unaowajali watu urejeshwe nchini humo.