Na Theophilida Felician, JamhuriMedia, Kagera
Katika kuelekea kufanyika zoezi la uchaguzi mkuu mnamo Oktoba 29, 2025 wananchi mkoani Kagera na kwingineko nchini wameaswa kutokujihusisha na mambo yenye viashiria vya uvunjifu wa amani ili kuepukana na vurugu zinazoweza kuhatarisha usalama nchini.
Ushauri huo umetolewa na mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Kagera Mzee Pius Ngeze akiwa ofisini kwake Manispaa ya Bukoba.
Mzee Ngeze ambaye ni mwenyekiti wa kwanza wa CCM Kagera tangu kuzaliwa kwa chama hicho mwaka 1977 na mbunge mstaafu wa Jimbo la Ngara amesema taifa linaelekea kufanya uchaguzi muhimu hivyo ni vyema amani ikaendelea kudumishwa kama ilivyo nyakati zote ili uchaguzi huo uweze kufanyika kwa amani na utulivu hatimaye kuwapata viongozi.

Amesema kila mmoja kwa nafasi yake yapaswa kuihubiri amani hivyo anapojitokeza mwenye kuhubiri maneno yenye chokochoko wananchi hawanabudi kumpuuza kwani hana nia njema na amani ya taifa ambayo imekuwa tunu kwa muda mrefu.
Aidha ameyataja madhara yatokanayo na uvunjifu wa amani hususani watu kukimbia nchi, kupoteza maisha pamoja na kupoteza mali na hatimaye kushi maisha ya mahangaiko ambapo ametolea mfano wa nchi zinazopakana na Tanzania kupitia mipaka ya Mkoa wa Kagera zilizokwisha yapitia machungu ya kuivunja amani ambazo ni Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya.
Hata hivyo amewasihi wananchi kuhakikisha wanakuwa watulivu hadi siku ya uchaguzi na wajitokeze kuwachagua viongozi wanaowafaa ili kuwaletea maendeleo kuhu akiwakumbusha CCM kukazana na kuzitafuta kura za wagombea ngazi zote kwa wananchi bila kujali itikadi za vyama vyao kwani wana CCM pekee bado hawatoshi kupata ushindi kwa viongozi waliowateua.
Amehitimisha akivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa namna vilivyosimama imara katika kuilinda amani ya nchi na wananchi wake kwa ujumla.