Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Arusha
Katika jitihada za kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi nchini, Mratibu wa Program ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK) Bw. Elia kamihanda amewataka wawakilishi wa wananchi kwenye zoezi la urasimishaji makazi katika kata ya Muriet mkoani Arusha kushirikiana na viongozi wa mitaa ili kuongeza kasi ya umilikishaji.
Bw. Kamihanda amesema hayo tarehe 17 Oktoba 2025 alipokutana na wawakilishi wa wananchi wa mitaa inayoshiriki zoezi la urasimishaji katika kata ya Muriet pamoja na viongozi wa mitaa hiyo wakati wa Klinik ya Ardhi ili kujadili namna bora ya kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi katika mitaa iliyofanyiwa urasimishaji.
Katika kata ya Murieti mitaa mitano imefanyiwa urasimishaji makazi holela ambapo jumla ya viwanja 18,886 vimetambuliwa huku viwanja 14,562 vimeidhinishwa kupimwa.

Mitaa iliyofanyiwa urasimishaji katika kata hiyo ni Mlimani, Msasani, Muriet, FFU pamoja na mtaa wa Mashariki.
‘’Kupitia Klinik ya Ardhi tumeona tukutane na wawakilishi wa wananchi ambao mitaa yao inashiriki zoezi la urasimishaji pamoja na viongozi wa mitaa ili kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunakamilisha huduma ya umilikishaji kwa haraka’’. Amesema Bw. Kamihanda
Amesema, zoezi la urasimishaji makazi holela lina manufaa makubwa kwa kuwa wananchi watapata usalama wa milki za kusimamia haki zao kupitia nyaraka za milki.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo wa Program ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK) wamefanya tathmini na kubaini changamoto kadhaa zinazosababisha kusuasua kwa zoezi la umilikishaji hivyo wamekubaliana kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo vikao vya uhamasishaji ambapo ameweka wazi kuwa, ni matumaini yake mikakati hiyo itasaidia kukamilisha zoezi.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendesha Klinik Maalum za Ardhi maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza kasi ya umilikishaji pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Huduma zinazotolewa kupitia Kliniki hizo ni pamoja na utoaji hati milki za ardhi papo kwa hapo kwa waliokamilisha taratibu za umiliki, utoaji elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo wa utoaji huduma za ardhi kidigiti (e-ardhi) na usaidizi wa ufunguaji akaunti ya mwananchi katika mfumo wa e-ardhi pamoja na kupokea, kusikiliza na kutatua migogoro za ardhi kiutawala.

