Na Mwandishi Maalumu, Arusha
Wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo ya mishipa ya damu kutanuka miguuni pamoja na wanaohitaji kuwekewa njia za kusafisha damu wameombwa kujitokeza katika kambi maalumu ya matibabu ya magonjwa mbalimbali inayoendelea katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ili kupata huduma za kibingwa kwa karibu.
Wito huo umetolewa leo na daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo na Mishipa ya Damu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Alex Joseph wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma zinazotolewa katika kambi hiyo.
Dkt. Alex alisema wagonjwa wenye matatizo ya figo wanapatiwa huduma ya kuwekewa njia za kusafisha damu, kitaalamu zikijulikana kama fistula na permanent catheter huduma ambazo mara nyingi hupatikana katika hospitali chache za rufaa.
“Katika kambi hii tunatoa pia huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya upasuaji wa mishipa ya damu, moyo na kifua. Tunawahimiza wananchi wenye matatizo ya mishipa ya damu isiyopitisha damu vizuri kufika ALMC ili waweze kuhudumiwa,” alisema Dkt. Alex.
Aliongeza kuwa tangu kuanza kwa kambi hiyo, wametoa huduma kwa wagonjwa 25 wenye matatizo ya mishipa ya damu pamoja na wanaohitaji kuwekewa njia za kusafisha damu, ambapo wagonjwa saba tayari wamefanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri huku wengine wakiruhusiwa kurejea nyumbani.
Kwa upande wao wagonjwa waliopata huduma katika kambi hiyo walishukuru juhudi za wataalamu wa afya, wakisema huduma hizo zimewapunguzia gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
“Nimefurahi sana kupata huduma ya kuwekewa njia ya kusafisha damu hapa ALMC. Nimewekewa permanent catheter jana na leo nimeruhusiwa. Nawahamasisha wagonjwa wengine wenye uhitaji huu kufika hapa,” alisema Elifuraha Mbise mkazi wa Ngaramtoni.
Mariam Issa mkazi wa Kijenge alisema alipata taarifa za ujio wa madaktari bingwa wa watoto ALMC na kuamua kumpeleka mtoto wake kupimwa afya.
“Mtoto wangu amefanyiwa vipimo vya moyo na damu bila gharama. Nawaomba wazazi wenye watoto wenye matatizo mbalimbali wafike ALMC kwani huduma zinapatikana,” alisema.
Naye Simon Kivuyo mkazi wa Kiseriani, aliwashukuru wataalamu wa afya kwa huduma alizopata na kusema kuwa wamepima vipimo mbalimbali vikiwemo vya moyo. Aliwahimiza wananchi watumie fursa hiy kupima afya zao mapema.
Kwa muda wa siku mbili tangu kuanza kwa kambi hiyo wananchi 312 wamejitokeza kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali, yakiwemo ya moyo kwa watoto na watu wazima.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete akimuhudumia mwananchi wa Arusha aliyefika kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo inayofanyika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) iliyopo jijini Arusha.





