Na Philipo Hassan, JamhuriMedia, Arusha

Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA Musa Nassoro Kuji, amewataka Maafisa na Askari Uhifadhi wa Uhifadhi waliopo TANAPA Makao Makuu na Kanda ya Kaskazini kujiendeleza kielimu ili kuboresha ufanisi katika utendaji kazi.

Aliyasema hayo leo Julai 16, 2025, alipofanya kikao kazi cha Maafisa na Askari waliopo TANAPA Makao Makuu na Kanda ya Kaskazini, kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Kibo uliopo katika eneo la Makao Makuu ya TANAPA katika Jengo la Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Jijini Arusha.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Kuji alieleza umuhimu wa kujiendeleza kielimu, jambo ambalo linasaidia kuongeza ujuzi, maarifa ya kukabiliana na changamoto zinapojitokeza, kuboresha huduma nyakati za kuwahudumia watalii na kuwa wabunifu ili kuleta ufanisi mahali pa kazi.

“Katika utendaji wenu wa kila siku kama watumishi wa TANAPA, tunategemea sana maarifa na weledi wenu ili kuboresha utendaji kazi. Hivyo, kujiendeleza kielimu ni moja ya njia bora za kuongeza uwezo huo. Kuongeza ujuzi na maarifa hufungua fikra mpya, huwajengea watumishi ujasiri wa kukabiliana na changamoto zilizopo na kusaidia kutumia mbinu za kisasa katika uhifadhi pamoja na kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wateja,” alisema Kamishna Kuji.

Sambamba na hilo, Kamishna Kuji alitumia nafasi hiyo kuwapongeza Maafisa na Askari Uhifadhi wote waliopo katika Shirika kwa namna walivyojitoa katika kuhamasisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuzipigia kura hifadhi za Taifa ambazo ziliingia kwenye mchuano wa tuzo zilizoandaliwa na Mtandao wa “World Travel Awards – WTA 2025” ambapo TANAPA ilishinda tuzo 7 kati ya 27 zilizokabidhiwa kwa Tanzania.

Awali akimkaribisha Kamishna wa Uhifadhi, Naibu Kamishna wa Uhifadhi (Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara) Massana Mwishawa alieleza kuwa Maafisa na Askari wapo tayari kupokea maelekezo kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi ili kufikia malengo yaliyowekwa na Shirika. “Afande Kamishna tupo tayari kupokea maelekezo yako kwa ajili ya utekelezaji na tuna morali ya kutosha kuweza kufanya kazi kwa bidii na maarifa” alisema Kamishna Mwishawa.

Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Theophilo Alexander akishukuru kwa niaba ya Maafisa na Askari Uhifadhi waliohudhuria kikao hicho, alimshukuru Kamishna wa Uhifadhi kwa maelekezo aliyoyatoa ya kuboresha utendaji kazi pamoja na kuhamasisha Maafisa na Askari kujiendeleza zaidi kielimu ili kuongeza weledi, ubunifu, ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya Shirika.

“Afande tunakuahidi tutatimiza majukumu kwa weledi, bidii na ufanisi kama ambavyo umetuelekeza. Pia, tunashukuru kwa kutusisitiza kujiendeza kielimu kwa manufaa ya Shirika na Taifa kwa ujumla.”

Kikao hicho ni mwendelezo wa ziara za kikazi za Kamishna wa Uhifadhi katika hifadhi za Taifa kwa lengo la kutoa maelekezo ya kiutendaji, kufuatilia maendeleo ya shughuli za uhifadhi, utalii na kuimarisha utendaji ndani ya Shirika kwa ujumla. ‎