Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Bw. Abdul-Razaq Badru amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa bidii, weledi, uamunifu, ubunifu na ushirikiano katika ulinzi wa rasilimaliza za Wanyamapori na misitu ili kuenzi uhuru wa Tanzania Bara kwa vitendo.

Katika salamu zake za kuadhimisha miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania Bara kamishna Badru amesema hifadhi ya Ngorongoro imedhamiria kuendelea kuwa eneo muhimu la uhifadhi na utalii duniani na kusisitiza kila mtumishi kutimiza majukumu yake kwa malengo ya kimkakati na kutekeleza dira ya nchi ya 2050.

“Dhamira yetu kwa Ngorongoro ni kuendelea kuifanya kuwa Premium Safari Destination hivyo hatutomwacha mtu nyuma wala kukata tamaa katika kutimiza malengo hayo na tutahakikisha tunalinda rasilimali za Wanyamapori, misitu na malikale zilizopo Ngorongoro kwa wivu mkubwa kama ambayo mwasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Nyerere alituachia,”alisema Kamishna Badru.

Ameeleza kuwa katika maadhimisho haya ya miaka 64 ya uhuru wa Tanzania bara njia pekee ya Ngorongoro kuyaenzi ni kuongeza ufanisi katika nyanja zote za uhifadhi,utalii na kudumisha mahusiano thabiti kwa maendeleo ya jamii.

Katika kuadhimisha siku ya uhuru wa Tanzania Bara Maafisa na askari wa Jeshi wa Uhifadhi Ngorongoro wametumia siku hiyo kufanya usafi katika maeneo mbalimbali yaliyopo eneo la hifadhi ya Ngorongoro ili kuendelea kuweka mandhari ya kuvutia kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.

Tanzania bara inaadhimisha miaka 64 ya uhuru uliopatikana tarehe 09 Desemba mwaka 1961 chini ya uongozi thabiti wa baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere.