Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Jeshi la Magereza limesema kampeni ya kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, imeleta manufaa makubwa kwa wafungwa na mahabusu zaidi ya 12,000 katika magereza mbalimbali nchini.
Kati ya waliofikiwa na kampeni hiyo, mahabusu 6,900 wametoka magerezani baada ya kupata usaidizi huo wa kisheria.
Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza (CP), Nicodemus Tenga amesema hayo mjini Morogoro katika taarifa yake kwenye ufunguzi wa awamu ya pili wa mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa sheria na urekebu wa jeshi kuhusu huduma za msaada wa kisheria, mapokezi ya wafungwa magerezani na adhabu mbadala.

Mafunzo hayo ya awamu ya pili yatakayofikia tamati Juni 13, yamefunguliwa na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, ambaye amewakilishwa na Naibu Katibu Wizara hiyo, Dk Franklin Rwezimula.
Kamishna wa Sheria na Undeshaji wa Magereza amesema, kwa minajili hiyo, idadi ya wafungwa kwenye magereza kwa mwaka 2021 ilikuwa zaidi ya 32, 000 lakini kwa mwaka 2025 hadi June 09, 2025 imepungua hadi 26,896.

“Kwa uwiano tuliokuwa nao kipindi hicho tulikuwa na wafungwa na mahabusu nusu kwa nusu lakini tunavyoongea sasa hivi wafungwa ni asilimia 75, na mahabusu ni asilimia 25,” amesema Tenga.
Kamishna Tenga amesema kutokana na mafunzo hayo, jeshi litaweka uratibu wa ufuatiliaji wa namna ambao wale waliopewa mafunzo watakavyoweza kuboresha utendaji wao wa kazi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji haki wa Wizara ya Katiba na Sheria, Jane Lyimo amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa kuhusu haki za binaadamu, usimamizi haki za wafungwa, utekelazaji wa adhabu mbadala na usimamizi wa mikataba.
“Wizara inatarajia kutoka kwenu kuzingatia haki za binadamu, kujenga mfumo wa haki, unatendaji kazi kwa ufanisi, uwazi na kwa kutumia ushahidi wa kisheria” amesema Lyimo.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa mafunzo hayo yamefanyika kwa awamu mbili yakihusisha jumla ya wanufaika 290 na kwamba hiyo ni kuonesha dhamira ya serikali katika kuimarisha mnyororo wa haki jinai.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Naibu Katibu Wizara hiyo Dk Rwezimula amesema kuwa Jeshi la Magereza limebeba dhamana kubwa isiyopaswa kubezwa, dhamana ya kusimamia hatua ya mwisho kabisa ya mnyororo wa haki jinai.
Dk Rwezimula amesema jukumu hilo linahitaji ujuzi wa kitaalamu, uelewa mpana wa sheria mbinu za urekebu wa tabia, uadilifu hali ya juu na uwezo kufanya kazi katika mazingira yenye changamoto mbalimbali.
Naibu Katibu mkuu huyo amesema katika dunia ya sasa inayokumbwa na mabadiliko ya kasi katika nyanja mbalimbali hususani kiusalama, kijamii na kisheria ni wajibu wa jeshi hilo kama Taifa kuwekeza kwa makusudi katika uimarishaji wa uwezo wa watumishi wa umma.
