Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Benki ya Tanzania (BoT) imesaini mikataba na Kampuni za Uchimbaji Madini za Geita Gold Mine (GGM), Buckreef Gold Ltd na Shanta Ltd ya kununua kiasi kisichopungua asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa.

Huo ni utekelezaji wa Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, Sura ya 123.
Hafla ya utiaji saini mikataba ya uuzwaji dhahabu imefanyika mapema wiki jijini hapa na kushuhudiwa na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwigulu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wenye maono na ambao umechochea kukua kwa hifadhi ya dhahabu ya BoT, hali itakayosaidia kuimarisha uchumi wa Tanzania.

โ€œSerikali kupitia Wizara ya Fedha itaendelea kuhakikisha inaiwezesha Benki Kuu katika ununuzi wa dhahabu ili kuongeza akiba ya nchi ya โ€˜๐™ข๐™ค๐™ฃ๐™š๐™ฉ๐™–๐™ง๐™ฎ ๐™œ๐™ค๐™ก๐™™โ€™.

โ€œNinampongeza Waziri Mavunde kwa usimamizi mzuri wa sekta ya madini mpaka kufikia hatua hii, ninaamini kwa miaka michache ijayo, nchi yetu itakuwa miongoni mwa zile zenye akiba kubwa ya hifadhi ya dhahabu kupitia Benki Kuu,โ€ amesema Mwigulu.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mavunde, amezipongeza kampuni zote za uchimbaji na usafishaji madini kwa kusaini mikataba hiyo ambayo ina matokeo makubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania na kuchochea uongezaji thamani madini nchini.


Mavunde amesema hatua ya BoT kununua dhahabu kupitia wachimbaji wadogo na wakubwa itaiweka Tanzania kwenye ramani ya Afrika kuwa miongoni mwa nchi 10 zenye hifadhi kubwa ya dhahabu Benki Kuu.

Akitoa taarifa ya awali, Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba, amesema hatua hii itasaidia kuimarisha uchumi na shilingi ya Tanzania.

โ€œBoT imejipanga kukuza hifadhi ya dhahabu kwa kuendelea na ununuzi kila mwaka ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwa na hifadhi kubwa itakayoihakikishia Tanzania uchumi imara,โ€ amesema Tutuba.

Amesema mpaka sasa BoT imeshanunua tani 5.02 za dhahabu, lengo likiwa kununua tani sita kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Malipo yote yamefanyika ndani ya saa 24.