Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amemtaka Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, kuhakikisha anasimamia kwa karibu malipo ya wakulima wa kahawa ili kuwalinda dhidi ya ucheleweshaji wa fedha zao unaofanywa na baadhi ya kampuni zinazonunua zao hilo.
Kapinga, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, ametoa maelekezo hayo mapema wiki hii alipokuwa akizungumza katika kikao na viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Amesisitiza kuwa zao la kahawa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Wilaya ya Mbinga na chanzo kikuu cha maisha ya wananchi wengi, hivyo Serikali haitavumilia kuona watu wachache wanaitia doa kutokana na uzembe au kushindwa kusimamia ipasavyo sheria na kanuni ili wakulima walipwe fedha zao za mauzo ya kahawa kwa wakati.
Katika maelekezo yake, Waziri Kapinga amemwagiza Afisa Ushirika wa wilaya hiyo, kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati bila visingizio, huku akiwataka watumishi kutotumia masuala ya ukomo wa malipo kama kisingizio cha kuwakandamiza wakulima.
Kwa upande mwingine, Waziri Kapinga amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, kufanya tathmini upya ya kampuni ya Mamba Coffee ili kubaini kama inastahili kuendelea kupewa kibali cha kununua kahawa, kutokana na malalamiko ya ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, amesema kuchelewesha malipo ni sawa na kuwarudisha nyuma wakulima na maendeleo yao.
Vilevile, amewahimiza viongozi wa vyama vya ushirika kukaa vikao na kufanya maamuzi muhimu mapema kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo, ili kuzuia migogoro inayoweza kuepukika.
Pia ametoa onyo kali dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za ushirika, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kutumia fedha hizo kwa maslahi binafsi hatavumiliwa.






