Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Judith Kapinga, ameipongeza Tume ya Ushindani Tanzania (Fair Competition Commission (FCC)) kwa juhudi zake za kuhamasisha na kulinda haki za mlaji nchini.
Judith ameyasema hayo wakati wa maazimisho ya siku ya haki za mlaji
duniani ambayo yalifanyia Johari Rotana
Dkt Judith amesema pongezi hizo zinatokana na shughuli mbalimbali
zilizofanyika katika kipindi chote kuelekea maadhimisho ya Siku ya Haki za Mlaji, katika kuhamasisha jamii kwa njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari
Amesema maazimisho hayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Machi. Lengo likiwa ni kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kulinda haki za walaji na kukuza soko lenye ufanisi, uwazi na misingi ya haki.
Ameeleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu
isemayo “Bidhaa salama, imani kwa mlaji,” ambayo inasisitiza umuhimu wa kuhakikisha bidhaa na huduma zinazotolewa sokoni ni salama, zinazingatia viwango, na zinakuwa na ubora unaokubalika ili kujenga
imani kwa walaji.
Kapinga amedai walaji ni mhimili muhimu wa uchumi wa taifa lolote, kwani bila walaji uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma hauna maana. Hivyo, kulinda haki za walaji ni sehemu muhimu ya kujenga uchumi imara na ushindani wenye tija ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya
uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mazingira
rafiki ya kibiashara pamoja na kuimarisha mifumo ya kumlinda mlaji
dhidi ya vitendo visivyo vya haki katika biashara.
Aidha, amesema serikali imeipatia FCC jukumu la kisheria la kuhakikisha masoko yanafuata misingi ya ushindani wa haki pamoja na kushughulikia malalamiko ya walaji kwa ukamilifu—jukumu ambalo awali
lilikuwa chini ya mahakama.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema taasisi hiyo imeendelea kufanya kampeni za kuelimisha jamii katika mikoa mbalimbali kupitia vyombo vya habari, ikiwemo vipindi vya redio, mihadhara ya umma na majadiliano na wadau.
Amesema elimu hiyo inalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kutambua
bidhaa salama na huduma bora, pamoja na kujiepusha na udanganyifu.
Ameongeza kuwa bado kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kutoa elimu kwa
walaji kutokana na wengi kutofahamu haki zao za msingi.
Kapinga pia ametoa wito kwa wafanyabiashara, wasambazaji na wauzaji
kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na viwango vinavyolinda
walaji. Amesema biashara inayozingatia usalama wa bidhaa, uwazi wa
taarifa na haki za walaji hujenga uaminifu kwa wateja na uimara wa
biashara yenyewe.
Aidha, amewataka walaji kuwa makini, kuuliza maswali na kutoa taarifa
kwa mamlaka husika wanapokutana na bidhaa zisizo salama au vitendo
visivyo vya haki. Amesisitiza kuwa walaji wenye uelewa sahihi ndio
msingi wa soko lenye uwajibikaji na uwazi.
Kwa upande mwingine, FCC imefanya utafiti maalum kuhusu biashara
mtandaoni nchini Tanzania, ambao unatarajiwa kusaidia katika masuala
ya kisera na kisheria, pamoja na kudhibiti bidhaa bandia sokoni.
Hata hivyo, Kapinga amesisitiza kuwa juhudi za kupambana na bidhaa
bandia bado hazijatosha, na kuitaka FCC kuongeza mikakati madhubuti
ili kulinda walaji dhidi ya bidhaa hizo.




