Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media-Muleba
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, Nazir Karamagi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ukarabati mkubwa uliofanywa katika bandari za Bukoba na Kemondo kuwa utasaidia kuondoa changamoto za usafiri kwa wananchi.
Karamagi ametoa kauli hiyo alipopewa nafasi ya kusalimia wakati wa mkutano wa kampeni za mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 15,2025.
Amesema ukarabati huo utasaidia kwa kiwango kikubwa kuanza kupokea meli kubwa za mizigo ambayo itasafirishwa kwenda Mwanza na nchi za jirani.
“Hatua hii ni kubwa sana kwetu, tunaamini sasa bidhaa mbalimbali zitashuka bei na kurahisisha maisha ya wananchi,”amesema.
Kuhusu uwanja wa ndege, Karamagi amemwagia sifa Rais Samia kuutumia baada ya viongozi kutofanya hivyo.
“Wewe ni kiongozi shujaa, umetumia uwanja wetu wa ndege wa Bukoba, huku nyuma viongozi wengine hawakutumia,”amesema.





