Na Mary Margwe, JamhuriMedia, Tarime
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara Raymond John Ole Matinda, amedhamiria kuanzisha mpango wa ujenzi wa nyumba ya katibu wa jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Kamati Tendaji.
Akizungumza na mara baada ya kikao hiko, ambacho kimelenga kujadili mpango wa ujenzi huo, ambapo Matinda amesema kuwa lengo kuu la kikao hiko ni kuweka msingi wa mpango huo muhimu, ambao una dhamira ya kuboresha mazingira ya kazi mtumishi wa Jumuiya hiyo wilayani Tarime.

Matinda amesema suala la ujenzi wa nyumba za watumishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Jumuiya zake ni agizo la muda mrefu, hivyo tutahakikisha tunalitekeleza hili kama agizo lilivyohitaji,huku akisema wako nyuma ya muda.
“Tulikaa kikao cha Kamati Tendaji ambapo tulijadili kwa kina suala la ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya, hili ni jambo la msingi sana katika kuimarisha utendaji kazi wa mtumishi husika, hivyo tutahakikisha linatekelezeka ili kumrahisishia mtumishi kuondokana na Hali ya kupanga huko mitaani, hivyo kama Jumuiya tutasimama na hili kikamilifu” amesema Matinda.
Aidha Matinda amefafanua kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa mchakato wa muda mrefu wa kuhakikisha jumuiya ya wazazi wilaya ya Tarime inakuwa na miundombinu bora inayowezesha viongozi wake kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na si vinginevyo.

“Tumeamua kuanza kwa kuweka maono na mwelekeo sahihi. Tutazidi kushirikiana na wanajumuiya na wadau mbalimbali wa Maendeleo katika kuhakikisha tunalifikisha lengo hili mahali stahiki,” amesema Matinda
Hata hivyo Matinda aliongeza kwa kuwaomba wanajumuiya hiyo kuhakikisha wanampa ushirikiano katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Maendeleo wanayojiwekea, ili kuweza kufikia malengo waliyokusidia na si vinginevyo.
” Niwaombe tu ndugu zangu, kunipa ushirikiano wenu wa dhati kwangu, kama mnavyofahamu Mimi mwenyewe bila ya ninyi sitaweza, hivyo tushirikiane bega Kwa bega kuhakikisha mipango yetu tuliyojiwekea inakamilika tena Kwa wakati kabisa, ili tutoke hapo na kuendelea na shughuli zingine mbalimbali, kama mnavyofahamu shughuli zipo nyingi sana katika Jumuiya yetu ya wazazi” aliongeza Matinda huku akisema mshikamano, nidhamu na moyo wa kujitolea miongoni mwa wanachama ili kuhakikisha ndoto hiyo inatimia kwa manufaa ya jumuiya na chama kwa ujumla.
