Na Mwandish Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amesema kuwa Serikali inatambua jitihada za wabunifu wa nyenzo mbalimbali zinazosaidia kupunguza gesijoto inayotokana na matumizi ya mafuta kwenye vyombo vya moto.

Alisema hayo wakati wa wadau kutoka Jumuiya ya Vyombo vya Moto vitumiavyo Umeme Tanzania (TAEMA) pamoja na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya namna bora ya kuifanya huduma hiyo iwe endelevu.

Dkt. Muyungi alitoa wito kwa wadau hao kuendelea kuongeza wigo wa huduma ya usafirishaji kwa kutumia magari ya umeme kwa kuwa hivi sasa Tanzania imeanza kuzalisha umeme wa kutosha hususan kutoka Bwawa la Nyerere.

“Tunawahitaji sana ninyi wadau wa sekta hii ya usafirishaji wa vyombo vya moto vya umeme, mtumie fursa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwani mtasaidia katika kupunguza uzalishaji wa gesijoto,” alisisitiza.

Aidha, Dkt. Muyungi alipongeza mchango wa COSTECH katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hususan kupitia tafiti zake ikiwemo Programu ya Utafiti wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Pamoja na hayo alitoa wito kwa Tume hiyo kuwekeza kwenye teknolojia ya kukabiliana na maabdiliko ya tabianchi kuhakikisha inakuwa chanzo cha maarifa ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Pia, Katibu Mkuu huyo aliwaomba wadau waendeleee kufanya kazi kwa karibu na Serikali katika kuhakikisha nchi inakuwa na maendeleo endelevu pamoja na kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAEMA Dkt. Pius Chombo alisema malengo makuu ya Jumuiya hiyo ni TAEMA ni pamoja na kusaidia Serikali katika kutengeneza sera na mifumo ya kisheria inayowezesha ukuaji wa vyombo vya moto vinavyotumia umeme.

Aliongeza kuwa wana majukumu ya kuhimiza matumizi salama na ya viwango vya kimataifa ya teknolojia za magari ya umeme na miundombinu yake na kukuza ushirikiano wa sekta, uendelezaji wa ujuzi, pamoja na kuongeza thamani ya uzalishaji wa ndani.

Kikao hicho cha kilitoa fursa kwa sekta binafsi kushirikisha uzoefu wa vitendo unaotokana na uendeshaji wa vyombo hivi vya umeme, vituo vya kuchajia na huduma zinazohusiana sanjari na vipaumbele vya kitaifa katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, usafiri wa mijini, matumizi bora ya nishati na maendeleo ya viwanda.