Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Mbarali

Katibu wa Siasa na Uenezi wa Kata ya Miombweni, Sevia Dickson Ngubi, amekanusha vikali taarifa zinazodai kuwa kulitokea vurugu wakati wa zoezi la kura za maoni lililofanyika wiki iliyopita katika kata hiyo.

Akizungumza na vyombo vya habari, Sevia amesema taarifa hizo zinasambazwa na kikundi kidogo cha watu wenye nia ya kupotosha ukweli na kuchafua taswira ya mchakato wa kidemokrasia uliofanyika kwa utulivu.

Kwa mujibu wa Sevia, amesema zoezi hilo la kura za maoni lilifanyika kwa amani na utulivu mkubwa, bila tukio lolote la vurugu au uvunjifu wa amani. Wananchi walijitokeza kwa wingi kushiriki, na mchakato mzima uliendeshwa kwa uwazi na haki chini ya usimamizi wa kamati husika.

Amesema kuwa madai ya vurugu hayana msingi wowote na ni propaganda zinazoenezwa na watu wasiopenda maendeleo.

Ameongeza kuwa baada ya matokeo kutangazwa, mawakala wote waliridhika na matokeo hayo na kuwaomba wafuasi wao kuheshimu uamuzi wa wengi. Wananchi nao waliondoka kwa utulivu bila kuzuka kwa vurugu ya aina yoyote.

Katibu huyo amewataka wananchi kupuuza taarifa hizo za upotoshaji na kuendelea kudumisha amani, mshikamano na utulivu uliopo katika Kata ya Miombweni

Jimbo la Mbarali lina jumla ya kata 24, na katika kata zote hizo, uchaguzi wa kura za maoni ulifanyika kwa amani, utulivu na kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa na chama.

“Hakukuwa na dosari yoyote ya uvunjaji wa sheria, vurugu, au vitendo vyovyote vya kuashiria uvunjifu wa amani. Hili ni jambo la kujivunia na ni ushahidi tosha wa ukomavu wa kisiasa uliopo miongoni mwa wanachama wa chama chetu” alisema.