*Wana CCM wahoji kama kuna haja ya Kura za Maoni.
*Ni baada ya kuwataka wasihangaike na wengine zaidi ya Ulega kwenye ubunge.
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mkuranga
Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama cha Mapinduzi( NEC) Taifa na Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, amewazuia wana CCM katika jimbo la Mkuranga Mkoa wa Pwani, wasijitokeze kuchukua fomu ya kuwania Ubunge wa jimbo hilo, kwa kile alichoeleza kuwa Mbunge wa sasa Abdallah Ulega ana baraka za mwenyekiti wa chama hicho Taifa,Dk Samia Suluhu Hassan.
Chatanda ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati kuu ya CCM Taifa,yenye wajibu wa kupitisha jina moja kati ya majina matatu ya wanachama watakaotoka katika ngazi zingine za maamuzi kwenye kura za maoni ,alitoa kauli hiyo jana mjini Mkuranga akiwa katika ziara ya chama chake kwa ajili ya kukagua miradi ya Maendeleo.
Alisema kwa sasa kuna watu wanajipitisha katika Jimbo la Mkuranga wakiwa na nia ya kutaka kuwania ubunge na kwamba watu hao hawana sifa ya kuzidi mbunge wa sasa wa jimbo hilo kwa kuwa ameshaaminiwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan,hadi kupewa nafasi ya uwaziri .
Chatanda aliongeza kuwa wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi mkuu wana Mkuranga wanapaswa kujua kuwa Ulega ni chaguo la viongozi wa chama hicho hadi kuaminiwa na kupewa uwaziri na Rais Samia.

“Kwa wananchi wa Mkuranga chagueni viongozi walio bora msihadaike na wanaojipitisha pitisha mnao viongozi bora ndani ya wilaya yenu, kwa sasa wanaendelea na kazi zao hadi Rais atakapovunja baraza la Mawaziri ndipo kila mmoja atakuja kuchukua fomu,lakini nawaambieni na mtanikumbuka mkifanya makosa mtakuja kujuta katika kipindi cha miaka mitano,mkifanya makosa na kuchagua watu wanaojipitisha pitisha hawa mtakuja kujuta.
“Rais ameiamini Mkuranga kwa kuwapatia Waziri na kama wananchi wana CCM watakosea kutokumrudisha watakuja kujuta ni lazima niwe mkweli Ulega anatosha”alisema Chatanda.
Aliwaambia wana CCM hawapaswi kubadilisha wabunge kama koti kwa kuwa aliyepo ameshaaminiwa na Rais kwa nafasi ya juu zaidi.
Hata hivyo kauli yake hiyo ilizua sintofahamu kwa wana CCM walioongea na mwandishi wa Habari hizi na kuhoji haki ya watia nia wengine,ikiwa Chatanda kwa nafasi yake ya Mjumbe wa NEC Taifa,ameshaweka wazi jina la mtu watakayempitisha katika jimbo la Mkuranga.
“Mmoja wa wanachama wa cham,a hicho Jumbe Mkaange, mkazi wa Kiparang’anda,alisema Kauli ya hadharani ya Chatanda inalenga kuwazuia wanaCCM wengine kuwania ubunge katika jimbo la Mkuranga.
Aliomba viongozi wa kitaifa wa CCM wajitokeze na kuikana kauli ya Mwenyekiti wa UWT Taifa kwa kuwa tayari mwenyekiti wa CCM alishasema hana mgombea wake kwenye mfuko na watapitisha wale watakaochaaguliwa na wananchi katika vikao vya chini.
Hata hivyo katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa Mei mwaka huu jijini Dodoma,mwenyekiti wa CCM Taifa,Dk Samia Suluhu Hassan,alisema wataheshimu uamuzi wa ngazi za chini na kupitisha jina la mtu anayehitajiwa na wanachama wa eneo husika
mwisho