📌Wananchi waipongeza Serikali kwa makati huo

Wananchi Kijiji cha Usevya Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kuhakikisha wanafikiwa na nishati safi ya kupikia kwa bei ya ruzuku.

Wametoa pongezi hizo kijijini hapo Agosti 12, 2025 wakati wa zoezi la usambazaji wa majiko ya gesi (LPG) ya kilo sita na vichomeo vyake kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 kwa kila jiko.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea majiko haya yanakwenda kurahisisha maisha yetu, majiko haya pia ni mkombozi wa mazingira naamini ukataji wa miti unakwenda kupungua,” alisema Davis Majaliwa Mkazi wa Usevya.

Kwa upande wake Christina Sindano mkazi wa Kijiji cha Usevya alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika kampeni hiyo ambayo alisema inanufaisha wananchi wake hususan kina mama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Usevya, Focus Kapongwa alisema wananchi kijijini hapo wamekuwa na mazoea ya kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa lakini kufika kwa mradi kutapunguza ukataji holela wa miti.

“Tunashukuru kwa hii huduma, tumepata shida sana kwenye ununuzi wa mkaa kwani sasa hivi mkaa ni bei ghali na haya majiko yatatusaidia kupunguza gharama ya maisha,” alisema Kapongwa.

Akizungumza kuhusu mradi, Mtaalam wa Jinsia na Nishati wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt.Joseph Sambali alisema mradi huo kwa Mkoa wa Katavi unatekelezwa kwa kushirikiana na Kampuni ya Taifa Gas Limited ambapo jumla ya mitungi 3,255 ya gesi ya kilo 6 ikiwa na mafiga na viwashio vyake itasambazwa kwa bei ya ruzuku katika kila Wilaya ya Mkoa wa Katavi kwa bei ya ruzuku.

“Majiko haya yanauzwa kwa bei ya ruzuku gaharama zingine zimebebwa na Serikali lengo ni kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa gharama nafuu ambayo kila mwananchi anamudu,” alisema Dkt. Sambali

Alisisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA) ili kuepuka watu kujirudia kwani dhamira ni kufikiwa kwa kila mwananchi.

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Mlele, Yahaya Mbulu alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali ikiwemo ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao na kuhifadhi mazingira.

“Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele kwenye Niishati Safi ya Kupikia; inakadiriwa kuwa takribani watu 31,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati isiyo salama,” alibainisha Mbulu.

Alitoa wito kwa wananchi kuacha kuharibu mazingira kwa kukata miti badala yake wachangamkie fursa hiyo ya majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku.

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wameachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama.