Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wafanyakazi wa majumbani wametajwa kuwa nguzo muhimu ya ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi, huku jamii ikihimizwa kuheshimu na kuitambua kazi hiyo kama ajira yenye staha.
Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Rashid Ally Salim, wakati akifungua mkutano kuhusu mradi wa Urasimishaji wa Kitaaluma kwa Wafanyakazi wa Majumbani Tanzania.
Salim alieleza ni wakati wa kuitambua kazi ya nyumbani kama taaluma rasmi kwa kuzingatia maslahi na haki za msingi za wafanyakazi hao, kwa kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.
“Hawa ni watu muhimu sana kwa kuwa wanatunza familia zetu tunapokuwa kazini au kwenye majukumu mengine ya kimaendeleo, Ni wajibu wetu kuwapa heshima na kuthamini mchango wao,” alisema Salim.
Aliongeza kuwa upatikanaji wa mafunzo ya ujuzi kupitia vituo vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ni miongoni mwa hatua zitakazowawezesha wafanyakazi hao kujiendeleza, kujitambua na kujiamini zaidi katika taaluma yao.
Kwa upande wake, mwakilishi wa VETA, Abdala Ulomi, alisema tayari wafanyakazi wa majumbani 1,280 wamepatiwa mafunzo katika vyuo sita vya Tanzania Bara na vitatu vya Zanzibar, huku mtaala maalum ukiwa tayari umeandaliwa.
Ulomi alifafanua urasimishaji wa mafunzo hayo unalenga kuongeza ubora na hadhi ya kazi hiyo, akibainisha kuwa mahitaji ya wafanyakazi wa majumbani ni makubwa ndani na nje ya nchi, hivyo kuitambua kama taaluma rasmi ni hatua muhimu.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rose Upor, alibainisha asilimia 95 ya wafanyakazi wa majumbani ni wanawake, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuboresha mazingira ya kazi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
Upor alisema suluhisho ni kukuza utu na kuhakikisha mazingira bora ya kazi, pamoja na kuendeleza tafiti zitakazosaidia kuleta usawa na kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi wa Shirika la CVM Tanzania, Magesa Nathaniel, alieleza taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza mradi wa miaka mitatu uliolenga kukuza kazi zenye staha na kulinda haki za wafanyakazi wa majumbani.
Nathaniel alisema miongoni mwa shughuli walizofanya ni kuwajengea uelewa na uwezo wafanyakazi hao, pamoja na kuwaunganisha na chama cha wafanyakazi wa majumbani, CHODAWU, kwa ajili ya utetezi wa haki zao.
Mwakilishi wa CHODAWU, Asteria Gerald, alisema kutambuliwa rasmi kwa kazi ya majumbani kutachangia upatikanaji wa heshima, ulinzi na stahiki nyingine, akibainisha kuwa bado baadhi yao wanakumbana na unyanyasaji, ukatili na kufanya kazi kwa muda mrefu bila masharti rafiki.
Gerald aliitaka Serikali kuridhia Mkataba Na. 189 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), unaolinda haki, hadhi na usalama wa wafanyakazi wa majumbani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi za Taaluma za Kijinsia wa UDSM, Dk. Sara Kisanga, alisema wafanyakazi wa majumbani wanapaswa kutambuliwa, kulindwa na kuendelezwa kiujuzi ili waweze kufanya kazi zao kwa staha na kwa kuzingatia haki za binadamu.






