Na Mwandishi Wetu, Jamhuriedia, Zanzibar

KCB Bank Tanzania imefanya hafla maalumu ya Iftar katika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar, ikilenga kuimarisha mshikamano na wateja wake pamoja na wadau wa maendeleo katika msimu huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shariah ya KCB Bank Tanzania, Sheikh Khamis Mataka, amesisitiza umuhimu wa kufanya biashara kwa uadilifu, uwazi, na misingi ya kumcha Mungu, mambo ambayo ni nguzo kuu ya huduma za Sahl Banking.

Mataka alisema kuwa kupitia Sahl Banking, wateja wanapata huduma mbalimbali kama vile Murabaha (ufadhili wa faida badala ya riba), Qard Hasan (mikopo ya muda mfupi isiyo na riba), pamoja na akaunti maalum za Hijja na akiba.

Mataka aliendelea kusema, ‘tunayo pia programu ya uwezeshaji wa Vijana inayoitwa 2Jiajiri inayowapa vijana mafunzo ya ujasiriamali na ujuzi wa kiuchumi. Vile vile benki yetu imekuwa ikisaidia nyumba za watoto yatima visiwani Zanzibar’.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Juma Malik Akil (katikati) akishiriki Iftar iliyoandaliwa na KCB Bank katika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar, ikilenga kuimarisha mshikamano na wateja wake pamoja na wadau wa maendeleo katika msimu huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kushoto kwake ni Sheikh Khamis Mataka, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Shariah KCB SAHL na kulia kwake ni Sheikh Mahmoud Mussa Wadi, Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar.

Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, aliipongeza Benki ya KCB kwa nafasi yake kama daraja kati ya mfumo wa kibenki wa kawaida na mahitaji ya kimaadili ya jamii ya Zanzibar.

Alihimiza benki hiyo kuendelea kubuni bidhaa zinazoendana na dira ya serikali ya kuwa na uchumi wa kidijitali na jumuishi.

Hafla hiyo ya Iftari iliwakutanisha viongozi wa serikali, viongozi wa dini, na jumuiya ya wafanyabiashara, ikiwa na lengo la kujenga mshikamano kati ya KCB bank na jamii katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.