Serikali ya Kenya imetetea uamuzi wa Tanzania kuwakataa baadhi ya viongozi wa kisiasa na wanaharakati wa Kenya kuingia nchini humo, hatua ambayo imezua mjadala mkali katika kanda ya Afrika Mashariki.
Kupitia kwa Msemaji wake, Isaac Mwaura, serikali ya Kenya imesema kuwa Tanzania ina haki kamili, kama nchi huru na mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ya kudhibiti nani anaingia ndani ya mipaka yake.
Mwaura amesema kuwa hakuna taifa jingine linalopaswa kuiwekea Tanzania shinikizo kuhusu masuala ya uhamiaji.
Viongozi waliokumbwa na zuio hilo ni pamoja na mwanasiasa wa upinzani Martha Karua na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya, Willy Mutunga. Haijafahamika wazi sababu za zuio hilo, lakini hatua hiyo imezua hisia tofauti ndani ya Kenya na kwingineko.
Serikali ya Kenya imesisitiza kuwa itaendelea kuheshimu mamlaka ya mataifa jirani na kuhimiza mazungumzo ya kidiplomasia katika kutatua masuala ya aina hiyo.
