Wizara ya Afya nchini Kenya imeibua wasiwasi juu ya mwelekeo unaoibuka wa watu kushiriki katika shughuli za kukumbatia miti kwa muda mrefu, huku ripoti zikionyesha kuwa baadhi ya washiriki wamepatwa na matatizo ya kiafya yaliyozidi kiasi cha kuhitaji kupelekwa hospitalini.

Akihutubia wakazi wa Ngiriambu, Jimbo la Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga, nchini humo, Katibu Mkuu wa Afya ya Umma, Mary Muthoni, alisema kwamba watu wanapaswa kufanya vipimo vya afya vya kina kabla ya kushiriki katika shughuli zinazohitaji nguvu za mwili, ili kubaini hali za kiafya zinazoweza kuhatarisha maisha yao.

Muthoni aliongeza kuwa shughuli zinazojulikana kuwa haziwezi kuwa hatari zinaweza kuwa hatari ikiwa mtu hajajiandaa ipasavyo, na kuwa wale wanaokusudia kushiriki mazoezi yanayohitaji nguvu nyingi wanapaswa kuhakikisha wako tayari vizuri na wamefanya mazoezi ya awali kabla ya kushiriki.

Awali kuna watu kadhaa nchini humo waliojaribu kukumbatia mti na kuanguka kwa sababu za kiafya.

Haya yanajiri baada ya msichana mwenye umri wa miaka 21, Truphena Muthoni kuvunja rekodi yake mwenyewe na kuweka rekodi mpya duniani kwenye Guinness World Record kwa kukumbatia mti kwa muda mrefu zaidi, saa 72 (yaani kwa siku tatu mfululizo).

Rekodi yake ya awali ilikuwa saa 48.Alisema amechagua njia hiyo ya maandamano kupinga ukataji ovyo wa miti na uharibifu wa misitu.

Ni hatua ambayo ilimpa umaarufu mkubwa hata katika rubaa za kimataifa na hadi kukabidhiwa cheo cha mazingira na Rais William Ruto.