Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amepongeza hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa meli nne unaoendelea katika Bandari ya Karema Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

Kihenzile ametoa pongezi hizo leo alipotembelea bandarini hapo kwa lengo la kujionea maendeleo ya mradi huo wa ubia kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kampuni ya Gold Voyage Logistics kutoka nchini China.

“Meli hizi zitakwenda kuongeza tija kwenye bandari zetu kwa sababu zitakuwa zinabeba mzigo kutoka nchi jirani kama vile Congo DR, Burundi na Zambia kuleta upande wetu kupitia bandari za Ziwa Tanganyika kabla ya kupokelewa Bandari ya Dar Es Salaam na kusafirishwa popote duniani,” Amesema Kihenzile.

Aidha Kihenzile ametoa mualiko kwa sekta binafsi kuja kuwekeza zaidi katika sekta ya uchukuzi ili kuongeza ufanisi katika usafiri na usafirishaji.

Awali akiwasilisha taarifa ya uendeshaji wa Bandari ya Karema Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Edward Mabula  amesema kuwa ujenzi wa meli tatu umekamilika na meli moja imefikia asilimia 90 na inatarajiwa kukamilika muda si mrefu.

Pia Mabula amesema kuwa tangu bandari hiyo kuanza imehudumia tani 15,000 za mizigo, meli saba na boti takribani 600 jambo linaloonesha kuwa bandari hiyo bado haijatumika ipasavyo lakini miundombinu itakapokamilika itakuwa na ufanisi unaotakiwa.