Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) anayesimamia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi ameeleza kufurahishwa na kazi nzuri ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Nzega Mkoani hapa.

Akiwa katika siku ya pili ya ziara yake, Kihongosi ametembelea na kukagua utekelezaji miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.5 iliyotekelezwa na serikali ya Awamu ya Sita katika Majimbo matatu ya Wilaya ya Nzega.

Mradi wa kwanza aliotembelea ni wa ujenzi wa mabweni 2 ya wanafunzi wa kike na kiume katika shule ya sekondari Puge, ujenzi wa vyumba 6 vya madarasa na matundu 10 ya vyoo, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 450.

Amebainisha kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo ambayo imefadhiliwa na Kampuni ya Barrick ni kichocheo muhimu sana cha kuinua ya taaluma katika shule hiyo, hivyo akatoa wito kwa walimu na wanafunzi kutumia vizuri miundombinu hiyo.

Mradi mwingine ni ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega uliogharimu zaidi ya shilingi 1.5 ambao umekamilika kwa asilimia 100 hivyo kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya kwa masaa 24.

Mradi wa mwisho kutembelewa ni ujenzi wa Chuo Cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika Halmashauri hiyo ambacho kitagharimu zaidi ya shilingi milioni 539 hadi kukamilika kwake.

Akihutubia umati mkubwa wa wakazi wa Wilaya hiyo katika uwanja wa stendi ya zamani Mjini humo baada ya kutembelea na kukagua miradi hiyo, ameeleza kuwa CCM imefanya kazi nzuri sana ya kuwaletea maendeleo.

‘Haya mazuri yote mnayoyaona yameletwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, hivyo endeleeni kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan (Mwenyekiti wa CCM Taifa) ili aendelea kuleta fedha za maendeleo’, amewasihi.

Amesisitiza kuwa amani na utulivu uliopo nchini ni matunda ya CCM na serikali yake na kuomba jamii isikubali kupotoshwa na watu wasioitakia mema nchi yetu ambao kila siku wanahamasisha vurugu na machafuko.