KATIBU wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Kenani Kihongosi amesema katika uchaguzi mkuu mwaka huu chama hicho ndicho chenye Ilani bora kuliko kipindi chochote kile kwani imebeba matumaini ya Watanzania nchini.
Akizungumza leo Oktoba 27,2025 mbele ya Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) pamoja na makundi mengine ya kijamii Kihongosi amesema matumani hayo ya Watanzania yamebebwa kuanzia vijana, wanawake na makundi mbalimbali wakiwemo kinababa, watoto na wazee wenye mahitaji maalum.
Amebainisha kwamba Ilani ya CCM inaingia mpaka kwenye familia palipo na kitovu cha ujenzi wa maadili ya taifa.”Hivyo tunaona ni kwa namna gani Ilani ya CCM imesheheni mambo mtambuka yanayokwenda kuleta majawabu ya Watanzania.
“Ilani ya CCM inatoa mwanga wa ajira na ustawi wa jamii. Inaleta suluhisho katika sekta ya afya.Inaahidi mapinduzi ya kiuchumi na uzalishaji. Dk. Samia anataka kuijenga Tanzania ambayo rasilimali zetu zinaongezwa thamani kuanzia ngazi ya wilaya na mikoa.
“Mgombea wetu amekuwa akisema atakwenda kuanzisha kongani za viwanda kuanzia kwenye wilaya, mikoa ili kuongeza thamani ya mazao ambayo yatakuwa yanazalishwa katika mikoa na wilaya husika. Hii itakwenda kufungua fursa kubwa kiuchumi.”
“Anafanya hivyo kwa kuwa anajua hatua hizo zitakwenda kumkomboa kiuchumi mwananchi kwa kumwezesha kuuza bidhaa badala ya malighafi.Ilani ya CCM ni mwanzo na mwisho wa kero za maji kwa kuwa serikali inakwenda kuanzia gridi ya maji ya taifa.
“Kuzalisha umeme megawati 8,000 ambayo ni mara mbili zaidi ya umeme uliokuwepo sasa. Katika sekta binafsi, Ilani inakwenda kupewa kipaumbele na nguvu kuliko wakati wowote nchini kwani CCM inataka kuendea muhula kwa kuleta tija katika kilimo kwa kulima na kufuga kisasa.
“Ndiyo maana kuna programu za chanjo ambazo serikali inatoa kwa wafugaji kuhakikisha mifugo nchi nzima inachanjwa ili wafugaji waweze kufuga kwa tija utakaoakisi maendeleo ya sasa,” amesema.
Akifafanua zaidi amesema katika sekta ya madini CCM imeahidi kuikuza, huku pia ikiahidi kuboresha makazi ya wananchi kwa kujenga miundombinu zaidi ili kila kona ya nchi ifikike kwa urahisi.
“Kwa msisitizo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imegusa kila eneo na huo ndiyo mwelekeo wa CCM ndani ya taifa hili,” amesema Kihongosi wakati anazungumza na makundi hayo ikiwa imebakia siku moja Wanzania kwenda kupiga kura katika Uchaguzi mkuu unaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.



