Jimbo la Darfur limekumbwa na janga kubwa la maporomoko ya ardhi ambapo kijiji kizima cha Tarasin kilichoko katika milima ya Jebel Marra kimesombwa kabisa na kusababisha vifo vya takriban watu 1,000.
Mamlaka za ndani nchini Sudan, Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kibinadamu yanaendelea kushughulikia athari za maporomoko ya ardhi yaliyotokea katika eneo la milima ya Jebel Marra jimbo la Darfur, ambapo kijiji kizima kimesombwa na mamia ya watu wamepoteza maisha.
Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Luca Renda, amesema katika taarifa kuwa Umoja wa Mataifa na washirika wake wengine wanajiandaa kutoa msaada kwa watu walioathirika na janga hilo.
Akinukuu vyanzo vya ndani, Renda ameeleza kwamba idadi ya watu waliopoteza maisha inakadiriwa kuwa kati ya 300 na 1,000.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, ameongeza kwamba kiwango kamili cha uharibifu bado hakijafahamika kutokana na ugumu wa kulifikia eneo hilo.
Timu za uokoaji kwa kushirikiana na wakaazi wa eneo hilo zinaendelea na juhudi za kuopoa miili, ingawa wanakumbwa na changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa vifaa na ukubwa wa janga hilo.
Umoja wa Afrika umezihimiza pande zinazohasimiana nchini Sudan kuweka silaha chini na kushirikiana kutoa msaada wa dharura.
Baraza la mpito la uongozi wa kijeshi chini ya usimamizi wa Jenerali Abdel Fattah al-Burhan limeahidi kuhamamisha raslimali zote zilizopo ili kusaidia waathiriwa, wakati serikali pinzani yenye makao yake Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini, imetangaza kuwa iko tayari kuanza juhudi za kutoa misaada.
