Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kupitia Kikundi Kazi cha Kilimo limekuja na maazimio kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta hiyo hapa nchini sambamba na kuifanya sekta hiyo kuchangia uchumi wa Taifa ipasavyo.

Akizungumza wakati wa mkutano wa pili uliojumuisha viongozi kutoka idara mbalimbali za Serikali na sekta binafsi jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kikundi Kazi hicho ambaye pia ni Katibu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, alisema lengo la mkutano huo lilikuwa kujadili mafanikio yaliyopo katika sekta hiyo na changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi kwa pamoja kati ya sekta hizo mbili.

“Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi tumeona haja ya kushughulikia changamoto zilizopo katika sekta ya kilimo kwa kupitia Baraza hili (TNBC) ambalo Mwenyekiti wake ni Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,”

Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha  Kilimo cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ambaye pia ni Katibu  Mkuu  Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, (katikati) akizungumza na wakurungenzi kutoka taasisi mbalimbali za Umma, sekta binafsi, wafanyabiashara na wakulima (hawapo pichani)  wakati  wa kikao cha pili cha kikundi kazi hicho kilichofanyika  jana  jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga na (kushoto) ni Mwenyekiti mwenza kutoka sekta binafsi ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi.

“Lengo ni kuona changamoto hizi zinaondoka na kukifanya kilimo kuwa na tija kwa wakulima na taifa kwa ujumla,” amesema.

Baadhi ya maazimio yaliyofikiwa na kikundi kazi hicho baada ya mijadala mbalimbali iliyoongozwa na Katibu Mkuu Mweli ni pamoja na kufanya mapitio/marejeo ya Sera, Mkakati, sheria na kanuni za kurahisisha upatikanaji wa mitaji ili taasisi za kifedha ziweze kuwakopesha wakulima kwa riba nafuu.

Mapendekeko mengine ni kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia changamoto zilizopo katika sekta ya usafirishaji na usimamizi wa ugavi wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa ajili ya masoko ya nje ya nchi.

Lakini pia kuimarisha mfumo wa takwimu za mahitaji na matumizi ya mbegu ambapo Serikali iendelee kuziwezesha taasisi mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ili kuzalisha mbegu bora zaidi.

Alisema maazimio mengine ni kujenga miundombinu ya umwagiliaji , viwanda na masoko katika maeneo ya kilimo cha mashamba makubwa (Block Farming) na kuimarisha kitovu cha masoko.

Wajumbe wa mkutano huo, pamoja na mambo mengine, pia walitoa wito wa kuimarisha na kuboresha mfumo unganishi wa kusimamia sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda vya usindikaji na kuimarisha mfumo wa utoaji taarifa na mrejesho wa Taasisi ya Afya na Ulinzi wa Mimea (TPHPA) kwa wakulima wa korosho na mazao mengine yanayouzwa katika katika soko la kimataifa.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Wanga (kulia) akizungumza na wakurungenzi kutoka taasisi mbalimbali za Umma, sekta binafsi, wafanyabiashara na wakulima  ( hawapo pichani) wakati  wa kikao cha pili cha kikundi kazi cha kilimo kilichofanyika  jana  jijini Dar es Salaam. (Katikati) ni Mwenyekiti wa Kikundi Kazi hicho ambaye pia ni Katibu Mkuu ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, na kushoto ni Mwenyekiti mwenza kutoka sekta binafsi, Dkt. Jacqueline Mkindi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa kikundi kazi hicho (anayewakilisha sekta binafsi) ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa TAHA ( inayojishughulisha na uzalishaji matunda na mbogamboga) Dkt. Jacqueline Mkindi, alieleza kuwa maazimio hayo yatafungua fursa nyingi kwa wakulima na wafanyabiashara wa kilimo kote nchini.

“Ninapongeza juhudi za Serikali, kupitia Wizara ya Kilimo, kwa kushirikiana na sekta binafsi kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya kilimo. Miradi kama ya ruzuku ya mbolea, bei nzuri ya mazao na mpango wa BBT (Jenga Kesho iliyo Bora) ni ya kuungwa mkono,” alieleza Bi Mkindi.

Naye Katibu wa kikundi kazi hicho na Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Wanga, alieleza kuwa miongoni mwa maazimio makuu ni pamoja na kuboresha huduma za ugani, kuhamasisha sekta binafsi kujisimamia yenyewe, kuboresha ulipaji wa ruzuku kwa wakati, kuendeleza sekta ya sukari kwa kukiimarisha chuo cha taifa cha bidhaa hiyo, kuimarisha chuo cha ubunifu na kuweka dirisha na namba moja ya malipo badala ya kila taasisi ya Serikali kudai stahiki yake ili kuondoa usumbufu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NFRA, Dkt. Andrew Komba amepongeza jitihada zinazofanyika na kusema kuwa Serikali (kupitia taasisi yake) imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye ununuzi wa nafaka kwa bei ya ushindani ili kuwasaidia wakulima.

“Kupitia uwekezaji huu, tunawakaribisha wadau wa kilimo kuwekeza kwenye ujenzi wa maghala katika mikoa ya Ruvuma, Songwe na Rukwa, kwani tunatarajia kununua tani nyingi za nafaka,” alisema Dkt Komba.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wakulima wa mazao mbalimbali wakiwemo wa Miwa, Pamba, Korosho, Kahawa na Chai ambapo wengi wao walipata fursa ya kuelezea changamoto mbalimbali zilizopelekea mkutano huo kuja na maazimio hayo.

“Tunaiomba Serikali iendelee kuongeza nguvu katika kilimo cha umwagiliaji kwani mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kwa miaka ya hivi karibuni,” alisema Mussa Hemed, mkulima wa Korosho kutoka mkoa wa Pwani.