Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete ameziagiza Mamlaka zote za nidhamu nchini ikiwa ni pamoja na Mamlaka za Maji kusimamia na kuzingatia ipasavyo Sheria, Kanuni na Taratibu katika usimamizi na uendeshaji wa masuala ya rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma ili kuiepushia Serikali hasara zisizo za lazima kwa baadhi ya michakato ya mashauri ya nidhamu kurudiwa.
Mhe. Kikwete alisema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Tume ya Utumishi wa Umma na Mamlaka za Maji nchini kuhusu utekelezaji wa sheria ya utumishi wa umma sura 298 na matumizi ya mfumo wa kielektroni wa kushughulikia rufaa na malalamiko na uwasilishaji wa taarifa za kiutumishi Tume.
“Nitumie fursa hii kuwakumbusha kuwa haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa kwa kuwa ukiukwaji wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma unachelewesha upatikanaji wa haki za Watumishi kwa wakati kutokana na mashauri hayo kurejeshwa na Tume ili kuanzishwa upya” alisema Mhe. Kikwete.
Katika hotuba yake, Mhe. Kikwete alibainisha kuwa jumla ya rufaa 52 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 na 2024/2025 zilizopokelewa kutoka Mamlaka za Maji na kutolewa uamuzi na Tume, ingawa rufaa 20 sawa na asilimia 38 ya rufaa zote zilizopokelewa katika kipindi hicho zilionekana kuwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma na kusababisha Tume kuzirudisha ili mchakato wa mashauri ya kinidhamu uanze upya.
Mhe. Kikwete alisisitiza kuwa asilimia hizo ni nyingi na aliipongeza Tume kwa kuandaa kikao kazi hicho chenye lengo la kutoa mafunzo ya namna bora ya kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi katika usimamizi na uendeshaji wa masuala ya rasilimaliwatu ili kuongeza ufanisi katika usimamizi na utoaji wa haki kwenye Utumishi wa Umma.
Tume ya Utumishi wa Umma ni chombo rekebu chini ya Ofisi ya Rais kilichoundwa ili kusimamia utoaji wa haki kwa kushughulikia rufaa na Malalamiko ya Watumishi wa Umma, kufanya ukaguzi, kutoa Miongozo na kutoa elimu kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira, Mamlaka za Nidhamu na Watumishi wa Umma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.






