Na Cresensia Kapinga, JamuhuriMedia, Songea
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Afya na maswala ya Ukimwi ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Elibariki Kingu, jana amezindua rasmi kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Songea Mjini, akihimiza wananchi pamoja na wanachama wa chama hicho kuona umuhimu wa kuwapigia kura za ndio Oktoba 29 mwaka huu mgombea wa nafasi ya Urais, wabunge na madiwani.
Akizungumza mbele ya wananchi katika viwanja vya shule ya msingi Kiblang’oma iliyopo Kata ya Lizaboni Manispaa ya Songea Kingu alitoa wito kwa wakazi wa Jimbo hilo kuendelea kuiamini CCM kutokana na utekelezaji wake wa Ilani ya 2020/2025 ambayo imetekeleza miradi ya maendeleo kwa vitendo ikiwemo sekta ya afya, elimu, barabara, umeme na maji.
“wananchi mmeona maendeleo makubwa chini ya uongozi wa chama Cha Mapinduzi ambao unaongozwa na Dk . Samia na Leo tunazindua kampeni zetu tukiwa na dhamira Moja tu ya kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na chama chetu” alisema Kingu.
Katika hotuba yake, Kingu pia alitumia nafasi hiyo kuinadi Ilani ya CCM ya 2025/2030 ambayo amesema kuwa imegusa kila sekta ikiwemo miradi ya kimkakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini Mwinyi Msolomi alimhakikishia Kingu kuwa chama kiko imara, na kinaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo unakuwa wa kihistoria.
Kwa upande wake Dkt. Damas Ndumbaro amewashukuru wananchi wa Jimbo hilo kwa kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi wa Kampeni na amewaahidi kuwa ataenda kutekeleza ilani ya chama Cha Mapinduzi kwa vitendo kama alivyofanya miaka mitano iliyopita ambapo alitumia nafasi hiyo kuelezea miradi aliyoitekeleza katika sekta ya afya, Maji,Elimu, Umeme,kilimo na miundombinu ya Barabara.
