Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameuawa katika shambulio kubwa dhidi ya Iran lililofanywa na Israel na Marekani, imesema televisheni ya taifa. Maafisa kadhaa waandamizi pia wameuawa.

Kifo hicho kimetilia shaka mustakabali wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu na kuongeza hatari ya kutokuwa na utulivu wa kikanda.

Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kifo hicho saa kadhaa kabla, akisema kinawapa Wairan “fursa kubwa ya kuichukua” nchi yao.

Televisheni ya serikali iliripoti kwamba kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 86 aliuawa katika shambulio la anga lililolenga makazi yake katikati mwa jiji la Tehran. Picha za satelaiti kutoka kampuni ya Airbus zilionyesha kuwa eneo hilo lililipuliwa kwa mabomu mengi.

Kifo chake ofisini kwake “kilionyesha kwamba alisimama miongoni mwa watu na kuwa mstari wa mbele katika majukumu yake, akikabiliana na kile ambacho maafisa wanakiita kiburi cha kimataifa,” ilisema televisheni ya taifa.