*Atangaza neema ujenzi wa taa 2,500, madaraja
*Akumbushia historia ya Mwalimu Nyerere

Na Kulwa Karedia,Jamhuri Media, Tabora

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),amehitimisha kampeni zake mkoani Tabora kwa kishindo.

Akizungumza na maelfu ya wakazi wa mkoa wa Tabora katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Nanenane Ipuli, Rais Samia amesema mkoa huo una nafasi ya kipekee katika historia ya kisiasa.


Amesema Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisoma katika mkoa huo na alipohitimu alirudi kufanya kazi hapo hapo.

“Mwalimu Nyerere alisona hapa, alipohitimu masomo kule Makerere alirudi kufundisha shule ya sekondari St. Marrys,”amesema
Amesema uamuzi wa kihistoria ulifanyika mkoani humo.

“Mwaka 1958 uamuzi yaliyofanywa na mkutano mkuu wa TANU kushiriki uchaguzi, maamuzi ambayo yalisogeza nchi yetu karibu na uhuru wake.”

Amesema huo ni udhibitisho namna chama hicho kilivyo na historia iliyotuka mkoani humo.

Alieleza kuwa mnara huo unaonyesha ukumbusho wa safari kuelekea uhuru wa kisiasa.

“Leo nchi yetu inaendeleza mapambano ya uhuru wa kujitegemea kiuchumi.

Tayari uhuru wa siasa tulishaupata mwaka 1961, leo tunakwenda katika mapambano ya kujitegemea uhuru wa kiuchumi.

“Uhuru wa kujenga taifa lenye uchumi jumuishi linalotegemea na linalozingatia ustawi wa watu wote. Ndiyo maana tunasema Kazi na Utu, Tunasonga mbele,”amesema.

Amesema chama hicho kinataka kujenga taifa linalojitegemea na linalozingatia.

“Maendeleo ni yetu na juu yetu wenyewe. Maendeleo tunayoyataka ni maendeleo ya watu, yaletwe na watu wenyewe, yaendelezwe na watu wenyewe na yawafuate watu kule walipo,” amesema.

Amesema hiyo ndiyo maana halisi ya uchumi jumuishi ambao CCM imedhamiria kuujenga kuleta maendeleo mijini na vijijini.

Amesema maendeleo hayo yaletwe na watu wenyewe ambao ni wananchi.


“Jana nilikuwa Kaliua mwaka 2023 lakini nimeingia Kaliua jana siyo ile kuna mabadiliko na maendeleo makubwa sana. Lakini pia maeneo yote nikipita maendeleo yanaonekana kwa macho tena kwenye sekta zote,”


Amesema sekta ya afya, elimu, maji, nishati na kilimo mambo makubwa yamefanyika.

Amesema serikali inatambua bado maendeleo hayo hayajatosheleza kwa sababu wananchi wanaendelea kuongezeka.

“Watu wanazaliwa wanakuwa wakubwa hivyo tunajua madarasa yatahitajika, vituo vya afya na matibabu yatatakiwa kila siku, maji yatahitajika, nishati utatakiwa kila siku kwa sababu maendeleo ya viwanda na mengine yanayohitaji umeme yanaendelea kukuwa ndani ya nchi yetu.

“Serikali ya CCM itakapopata ridhaa itasogeza karibu maji, umeme, kilimo na ufugaji.

Hata shughuli za uvuvi nazo zitajumuishwa,.
Amesema katika wilaya za Urambo na Kaliua, umeme ulikuwa hautoshelezi mahitaji ambapo serikali iliahidi kujenga kituo cha kupoza umeme na sasa tatizo hilo limemalizika.

Amesema serikali itajenga kituo cha kudhibiti mifumo ya usambazaji umeme eneo la Ziba wilayani Igunga ili kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji itakapokamilika, vituo hivyo vitadhibiti, kupoza na kusambaza nishati hiyo.

Amesema serikali iliahidi kufanya upanuzi na ukarabati kiwanja cha ndege Tabora kazi ambayo imefikia asilimia 95 huku kiwanja kikiendelea kutumika.

“Tabora tunakwenda kuwa na kiwanja kikubwa na kizuri cha kutua ndege kubwa zaidi,” alisisitiza.


Kuhusu sekta ya kilimo, alisema serikali inakwenda kuweka mkazo kutoa ruzuku kwa wakulima kuanzia mbolea, pembejeo na chanjo.

Asema serikali itakwenda kufanya maboresho ya minada, ujenzi wa majosho na kutoa zaidi chanjo ya mifugo.

“Upande wa kilimo cha mazao, tunakwenda kuendelea ujenzi na ukarabati wa skimu za kumwagilia ili wakulima waweze kuzalisha mara mbili kwa mwaka.

“Kuna miradi inayoendelea kutekelezwa itakapokamilika tunatarajia Mkoa wa Tabora uwe na maji ya kutosha. Na kila mwananchi apate maji ya kutosha,” amesema.

Amesema kupitia mradi unaotoa maji Ziwa Victoria na ule wa miji 28 utakwenda kuondoa changamoto ya maji ndani ya mkoa huo.

Amesema baadhi ya miradi hiyo, ni ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga.

Alisema mradi huo unapita katika wilaya za Nzega na Igunga, unakwenda kuzalisha ajira kwa vijana watakaokuwa na sifa za kufanyakazi katika mradi huo.

Amesema.mradi huo unapita wilaya za Uyui, Urambo na Kaliua ambapo vitajengwa vituo vya kushusha na kupakia abiria.

“Katika maeneo ya vituo maendeleo mbalimbali yatakuja, biashara zitakazowekwa kupitia sekta binafsi lakini pia maghala ya kuhifadhi bidhaa zitakazosafirishwa na reli hiyo.

“Hiyo ni ajira na fursa za biashara ambazo tungeomba wananchi wa Tabora wazitumie ili kukuza uchumi, kupata ajira na kuendeleza biashara,” amesema.

Kuhusu miundombinu, Samia amesema barabara za mijini na vijijini zitaimarishwa.

Amesema miundombinu hiyo iliimarishwa kuongeza bajeti ya Tarura kwa mwaka huu wa fedha kutoka sh. bilioni 700 hadi sh. trilioni 1.9 ili kufungua barabara vijijin ambapo kwa mkoa huo wanakuja na ujenzi wa barabara mpya

“Napenda kuwambia tunakuja na ujenzi wa barabara mpya ya mzunguko ya Tabora mji, tumeshaifanyia tathmini itakayokuwa na urefu wa kilometa 82.

“Lengo letu ni kuhakikisha magari yote yasiyokuwa na ulazima kupita ndani ya mji wa Tabora, yapite katika barabara hiyo ya nje.

“Tunataka Tabora yenye historia kubwa iwe na hadhi kubwa pia. Katika hatua nyingine ndani ya mkoa huu tutajenga madaraja 133.”

Amesema madaraja hayo yatajengwa katika barabara zilizojumuishwa katika Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025-30.

Amesema serikali itajenga taa za barabarani 2,500 na kusaidia kufungua fursa za kufanyabiashara saa 24 maeneo mbalimbali.