Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Wananchi wa Kata ya Zanka, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wameanza kuona mwanga mpya wa maendeleo kufuatia uzinduzi rasmi wa kiwanda cha kusindika na kuyeyusha madini ya Nikeli na Shaba kinachomilikiwa na kampuni ya Zhong Zhou.
Hafla ya uzinduzi huo imehusisha uwekaji wa jiwe la msingi, ikiongozwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa serikali, wachimbaji wadogo, wawekezaji na wananchi waliokusanyika kushuhudia hatua hiyo muhimu katika historia ya maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Akizungumza leo Agosti 26,2025 wakati wa hafla hiyo, Waziri Mavunde ameeleza kwa furaha kubwa kuwa hatua ya kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni ushahidi wa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha madini hayaondoki nchini yakiwa ghafi, bali yanaongezewa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
“Leo ni siku ya furaha sana kwangu binafsi na kwa Wizara ya Madini kwa sababu jambo tulilolisubiri kwa muda mrefu hatimaye limetimia,tumeacha kusafirisha udongo wala mawe, sasa tunachakata madini yetu hapa nchini,” amesema.
Waziri huyo amefafanua kuwa Serikali kwa sasa ina viwanda nane vinavyochakata dhahabu, huku kiwanda cha Chunya kikiwa tayari kinachakata madini ya shaba, na kwa upande wa Dodoma, kuna viwanda vitano vinavyojengwa kwa ajili ya kuongeza thamani ya madini mbalimbali.
Kulingana na Waziri Mavunde, uwepo wa viwanda hivyo utasaidia si tu kuongeza ajira, bali pia kupanua ujuzi wa Watanzania katika teknolojia ya uchakataji wa madini na kwamba kinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 300 za moja kwa moja, pamoja na fursa nyingine za ajira zisizo rasmi kupitia shughuli za usambazaji, huduma za kijamii na biashara ndogo ndogo zitakazozunguka kiwanda hicho.

“Aidha, wananchi watanufaika kwa kupatiwa ujuzi wa kisasa kuhusu usindikaji wa madini, hali itakayoongeza tija na ufanisi kwa wachimbaji wadogo na wajasiriamali wa eneo hili, ” amesema.
Mbali na ajira,amesema kiwanda pia kinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kupitia ushuru hatua itakayochangia kuboreshwa kwa huduma za kijamii kama elimu, afya na miundombinu.
Mavunde amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha wawekezaji wanazingatia ushirikishwaji wa wananchi na kuhakikisha faida za uwekezaji huo zinaonekana moja kwa moja kwa jamii inayowazunguka.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini amesisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya juhudi madhubuti za serikali katika kusimamia sera na sheria za madini na kuhakikisha kunakuwepo na mazingira rafiki ya uwekezaji.

“Miaka ya nyuma hili lilikuwa jambo gumu, lakini sasa tumefanikisha,Madini yanapo ongezwa thamani yanaleta tija katika kuongeza ajira, yanachochea mapato ya taifa na kuwanufaisha wachimbaji wadogo,” amesema.
Pia amewahamasisha wachimbaji wadogo kutumia fursa hiyo kujiendeleza, akisisitiza kuwa Serikali iko tayari kuwaunga mkono kwa kutoa elimu na vifaa ili kuongeza uzalishaji na ubora wa madini yao.
Aidha, ametoa wito kwa kampuni ya Zhong Zhou kuhakikisha inashirikiana kwa karibu na jamii ya Zanka na maeneo ya jirani, ili maendeleo haya yazidi kuwanufaisha Watanzania wengi zaidi.

Kwa mara nyingine, sekta ya madini nchini Tanzania imedhihirisha kuwa siyo tu chanzo kikubwa cha pato la taifa, bali pia ni msingi wa kuinua maisha ya wananchi wa kawaida pale ambapo rasilimali hizo zinatumiwa kwa tija na kwa manufaa ya wote.
Uzinduzi wa kiwanda hiki ni ushahidi tosha kuwa Tanzania sasa inasonga mbele katika dira ya kuongeza thamani ya rasilimali zake kwa maslahi ya Taifa na kufanikiwa kuingia kwenye Sera ya Madini ni maisha na Utajiri.