Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, mkoani Pwani, Silvestry Koka, amesema kata ya Pangani inakwenda kuwa kitovu cha maendeleo, akiwataka wananchi kutokiangusha Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu oktoba 29,2025.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Pangani, Oktoba 1, 2025, Koka alisema zaidi ya wapiga kura 14,700 waliojiandikisha katika kata hiyo wanapaswa kutumia haki yao kuchagua viongozi bora ili kuhakikisha CCM inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alieleza serikali inakwenda kuanzisha programu ya ujenzi wa viwanda katika kata ya Pangani, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira.
Aidha, alisema thamani ya ardhi imepanda na wananchi wasiwe na hofu kuhusu dhuluma za upangaji wa mji kwani serikali itasimamia haki na uwazi, hususan eneo la Mitamba ,Pangani.
Kuhusu sekta ya elimu, Koka alieleza serikali inatarajia kujenga shule ya sekondari katika eneo la Vikawe, pamoja na shule mpya ya awali na msingi Ubafu.
“Shule ya msingi Kidimu na Lumumba zitawekwa mazingira bora ya afya kwa kujenga matundu ya vyoo 33, maabara tatu za sayansi katika shule ya sekondari ya Pangani ili kuinua ufaulu wa masomo ya sayansi, kujenga hostel tatu, ,madawati 2,000 kwa shule za msingi na sekondari ili kuondoa changamoto ya upungufu wa samani mashuleni.

Vilevile Koka alieleza , CCM itaweka Historia kumalizia ujenzi wa tanki kubwa la maji, usambazaji wa maji tayari imefikia asilimia 4 na kiasi cha sh bilioni 89 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji Pangani.
Huduma ya afya, Koka alibainisha kuwa serikali itajenga zahanati katika maeneo ya Lumumba na Mkombozi, lengo likiwa ni kusogeza huduma, kituo cha afya Pangani kitaongezewa huduma ya mionzi na wodi nyingine za kisasa.
Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Mwalimu Mwajuma Nyamka, aliwataka wananchi waendelee kukipa imani Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa ilani ya 2025–2030 imesheheni mikakati madhubuti ya maendeleo.

Alisema wagombea wote wa CCM ni mahiri, na chama hicho kiko karibu na wananchi katika kutatua changamoto zao.
Mgombea wa udiwani kata ya Pangani, John Katele, aliwahimiza wananchi kuchagua timu yenye mshikamano, ambayo ina nia ya kuleta kasi ya maendeleo katika kata hiyo.


