Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza

WASHIRIKI takribani 1,000, wanatarajiwa kushiriki katika kongamano la nne la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza(Tanzania Monitoring, Evaluation and Learning Week).

Kongamano hilo litawakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo viongozi wa serikali, mabalozi, sekta binafsi, taasisi za elimu na vijana,ambalo litafanyika kwa siku nne jijini Mwanza kuanzia
Septemba 10 hadi Septemba 13, mwaka huu.

Akizungumza Septemba 9, 2025 na waandishi wa habari mkoani hapo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema kongamano hilo hutumika kama jukwaa la kitaifa linalowakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujifunza na kuimarisha mbinu bora za ufuatiliaji na tathimini (M&E) katika utekelezaji wa sera.

Mtanda amesema, ufuatiliaji na tathimini ni silaha muhimu kwa Serikali katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati,ubora na kwa thamani halisi ya fedha.

Amesema, kupitia ufuatiliaji na tathimini inayofanyika mara kwa mara kumesaidia kutekelezwa kikamilifu kwa miradi katika Mkoa wa Mwanza huku tija iliyokusudiwa kupatikana kwenye miradi hiyo na thamani ya fedha kuonekana.

“Miradi hiyo ina thamani ya Tsh.tirioni 5.6,iliyotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2021-2025 na kuwezesha kufanya uwekezaji mkubwa katika kujenga uchumi na kuboresha hali za maisha ya watu ikiwemo kuendeleza miundombinu ya kiuchumi na kijamii,” amesema Mtanda.

Aidha Mtanda ametaja miradi hiyo ya maendeleo kuwa ni pamoja na ujenzi wa daraja la JPM(Kigongo – Busisi),reli ya kisasa(SGR), miundombinu ya vivuko,hospitali ya kibingwa yenye hadhi ya Mkoa Wilayani Ukerewe, ujenzi wa barabara kupitia TANROADS na TARURA.

“Pia ujenzi wa soko kuu la kisasa Mjini Kati, mradi wa maji Butimba na ujenzi wa meli kubwa ya abiria na mizigo ya MV MWANZA, haya yote ni kielelezo tosha ya namna Serikali ilivyoufungua Mkoa wa Mwanza,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathimini ya utendaji wa Serikali,Sakina Mwinyimkuu,amesema, kongamano hilo ni la nne kufanyika nchini hapa,ambapo la kwanza lilifanyika mwaka 2022 mkoani Dodoma,na kufunguliwa na Waziri Mkuu ambaye alihimiza kuwa liwe endelevu.

Mwinyimkuu amesema, kongamano la pili lilifanyika mkoani Arusha,na la tatu lilifanyika Zanzibar mwaka jana na sasa ni la nne mkoani Mwanza,ambalo litakuwa na mijadala mbalimbali ya namna Serikali imefanikisha utekelezaji wa miradi.

Pia amesema, wamealika washiriki kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu,taasisi za Serikali na washiriki kutoka takribani nchi 18.

Aidha amesema, tathimini zilizopita zinaonesha kumekuwa na mwamko mkubwa katika eneo la ufuatiliaji na tathimini.

“Taasisi za umma zote kwa sasa zinafanya tathimini ya mipango mikakati ambayo imekuwa ikitekeleza.Tunaamini kupitia kongamano hili litaleta hamasa na kujenga utamaduni wa kufanya tathimini,pia naamini miradi mingi itaenda kuleta matokeo zaidi kwa nchi,” amesema Mwinyimkuu.