Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

ZAIDI ya madaktari bingwa wa saratani, wataalamu wa tiba mionzi, watafiti na watunga sera kutoka nchi zaidi ya 20 wanatarajiwa kushiriki kongamano la kwanza la kimataifa la saratani litakalofanyika jijini Dar es Salaam Februari 4-6, 2026.

Kongamano hilo, ambalo pia litawakutanisha washiriki zaidi ya 600 wakiwemo washirika wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia, ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI na Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya kongamano, Dk. Diwani Msemo amesema washiriki hao watajadili safari ya taasisi hiyo kwa miongo mitatu, kushirikishana ubunifu na kubuni mikakati mipya ya kudhibiti saratani nchini na kimataifa.

“Siku mbili za mwanzo, Februari 4 na 5, zitakuwa maalum kwa ajili ya kongamano, na Februari 6 tutahitimisha kwa kilele cha sherehe za miaka 30 ya ORCI,” amesema Dkt. Msemo.

Ameongeza kuwa kabla ya kongamano kutakuwa na shughuli mbalimbali kuanzia Januari 2026, zikiwemo majukwaa ya elimu kwa jamii na vipindi vya redio na televisheni kuhusu saratani.

Kwa mujibu wa Dkt. Msemo, ORCI imeendelea kuwa kituo kikuu cha matumaini kwa wagonjwa wa saratani nchini, ikitoa huduma za tiba ya mionzi, tiba dawa (chemotherapy), upasuaji, tiba ya nyuklia, uchunguzi, utafiti na huduma za mafunzo.

“Katika miaka 30 tumegusa maisha ya maelfu ya wagonjwa, tukajenga timu ya kitaalamu yenye weledi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa,” alisema.

Aidha, amesema taasisi hiyo itazindua Mpango Mkakati wa 2026–2030 wenye lengo la kupunguza vifo vinavyosababishwa na saratani kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.

Amebainisha pia kuwa ORCI kwa sasa inatumia teknolojia za kisasa ikiwemo mashine ya kugundua saratani iliyojificha kwa njia ya nyuklia, jambo linaloifanya taasisi hiyo kuvutia wagonjwa hata kutoka nje ya nchi wanaohitaji huduma bora kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Tiba Utalii kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Asha Mahita amesema saratani zinazoongoza kwa maambukizi duniani ni saratani ya mlango wa kizazi na matiti kwa wanawake, saratani ya tezi dume kwa wanaume pamoja na saratani ya koo.

“Takwimu zinaonyesha kati ya watu 100,000 wanaojitokeza kupima, 68,000 hukutwa na viashiria vya saratani. Hivyo kongamano hili litatoa fursa ya kujadili namna bora ya kuongeza elimu ya kinga na uchunguzi wa mapema,” amesema.

Mbali na hayo, ORCI imezindua tovuti rasmi kwa ajili ya maadhimisho hayo, ikitoa wito kwa Watanzania kuitumia kupata taarifa na huduma zinazohusiana na saratani.